Serikali kutafutia bandari biashara

Serikali kutafutia bandari biashara

Na ANTHONY KITIMO

SERIKALI imepanga kutuma wajumbe kutafutia biashara bandari ya Lamu katika mataifa jirani kuanzia wiki hii.

Hii ni baada ya meli ya tano ya mizigo kutia nanga katika bandari hiyo Jumamosi, tangu ilipofunguliwa Mei 2021.

Meli ya Uholanzi inayofahamika kama Mv Seago inayomilikiwa na kampuni ya Maersk, ilitia nanga Lamu baada ya kutoka katika Bandari ya Salalah, Oman, kupakua makasha 100 ya mizigo iliyonuiwa kuelekea Zanzibar.

Meli hiyo iliyo na urefu wa mita 294 ni refu zaidi kuwahi kutia nanga katika bandari hiyo kufikia sasa, na ni ya pili kwa urefu zaidi kuwahi kutia nanga katika bandari za Kenya.

Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani, alisema meli nyingine inatarajiwa kufika wiki mbili zijazo, ishara kuwa makampuni mengi yana imani na uwezo wa bandari hiyo kuendeleza biashara zao kimataifa.

“Tangu bandari ya Lamu ilipofunguliwa, tumepiga hatua na bandari hii imedhihirisha ina nafasi bora zaidi kwa usafirishaji mizigo kimataifa,” akasema.

Akiandamana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA), Bw John Mwangemi, waziri alisema wajumbe watatumwa Ethiopia na Sudan Kusini kutafutia soko bandari hiyo.

Kamishna wa Forodha na Usimamizi wa Mipaka katika Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA), Bi Lilian Nyawenda, alisema kwa sasa mamlaka hiyo inatilia maanani zaidi kuwapa imani wafanyabiashara kuhusu uwezo wa Kenya kuidhinisha bidhaa kupitia nchini kwa haraka.

“KRA imeongeza wafanyakazi na vifaa katika afisi zake mipakani ili uidhinishaji wa bidhaa ufanywe haraka. Wawekezaji wakiwa na imani kwetu, mapato yataongezeka kwa urahisi,” akaeleza.

Mkurugenzi Mkuu wa Maersk ukanda wa Afrika Mashariki, Bw Carl Lorenz, alihimiza kampuni nyingine kuungana kukuza sekta ya uchukuzi wa mizigo kwa manufaa ya uchumi.

Mradi wa bandari ya Lamu ulikuwa mojawapo ya ile ambayo Rais Uhuru Kenyatta alikusudia kukamilisha kabla aondoke mamlakani baada ya uchaguzi ujao wa urais.

Kufikia sasa, Zanzibar na nchi zilizo Mashariki ya Mbali zimeibuka kuwa soko kuu la bandari ya Lamu.

Mapema Julai, meli ya kwanza ya shirika la CMA CGM ilikuwa ya kwanza kutia nanga Lamu kutoka Soviet Union, ambapo ilibeba makasha 50 yaliyokuwa yametoka Zanzibar.

Bandari hiyo haijaanza kupokea mizigo kutoka kwa malori kwa sababu ujenzi wa barabara kuu zinazotegemewa haujakamilika.

Wakati huo huo, KPA ilisema iko tayari kuhudumia meli aina yoyote katika bandari hiyo badala ya kukamilisha kuezeka mashine zote zinazohitajika kupakia na kupakua mizigo mikubwa.

You can share this post!

Serge Gnabry awabeba Bayern Munich dhidi ya Cologne kwenye...

Yordenis Ugas wa Cuba amnyuka Many Pacquiao wa Ufilipino na...