Habari Mseto

Serikali kutenga Sh1.1 bilioni zaidi kwa ukarabati wa feri

November 6th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI inapanga kutenga Sh1.1 bilioni zaidi katika mwaka huu wa kifedha kugharimia ukarabati wa feri ambazo hutumika katika kivuko cha Likoni na kile cha Mtongwe baada ya kubainika kuwa ni hatari kwa usalama wa wasafiri.

Waziri wa Uchukuzi James Macharia akiwa mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC), aliiambia Jumanne kwamba wizara yake imetuma maombi kwa Wizara ya Fedha ikitaka iruhusiwe kusimamisha utekelezaji wa miradi isiyo ya dharura na kuelekeza fedha hizo kwa Shirika la Feri Nchini (KFS).

“Haja yetu kuu ni kuzuia maafaa kama ilivyoshuhudiwa Septemba. Hii ndiyo maana tumewasilisha ombi kwa Wizara ya Fedha ili kuruhusiwe kuhamisha fedha kutoka idara zingine na kutumia pesa hizo kukaribati feri zote sita zinazomilikiwa na KFS,” akasema Bw Macharia.

Waziri huyo aliungama mbele ya kamati hiyo, inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sheriff Nassir, kuwa feri zote sita zinazomilikiwa na shirika la KFS haziko katika hali nzuri japo zinaendelea kutumika.

“Huu mpango wa ukarabati wa vyombo hivi utakuwa wa muda tu huku tukiendeleza mipango ya muda mrefu ya kufanikisha uchukuzi katika vivuko vya Likoni na Mtongwe. Mojawapo ya hatua hizo ni ujenzi wa daraja la juu kwa juu, maarufu kama Mombasa Gate Bridge kwa gharama ya Sh60 bilioni,” akasema Bw Macharia.

Wiki jana, Meneja Mkurugenzi wa KFS Bakari Gowa aliungama mbele ya kamati hiyo ya PIC kwamba feri zote sita zinazomilikiwa na shirika hilo hazijatimiza viwango vya usalama vinavyokubalika na Shirika la Kimataifa la kuidhinisna vyombo vya baharini, Lloyd Register Group Ltd.

Alisema feri za kwanza kukataliwa na shirika hilo mwaka 2007 ni MV Harambee, MV Nyayo na MV Kilindi kwa misingi kuwa ni kuukuu na zimetumika kwa miaka 30 badala ya angalau miaka 20 inavyohitajika kisheria.

Feri ya MV Harambee ndiko kulikotokea ajali katika kivuko cha Likoni ambapo Mariam Kighenda na bintiye Amanda Mutheu walikufa maji baada ya gari lao (walimokuwa ndani) kuteleza na kutumbukia baharini.

Gari hili liliopolewa baada ya siku 13 katika operesheni iliyoendeshwa na wapigambizi wa asasi za humu nchini ambao walipapa usaidizi kutoka kwa wataalamu kutoka Afrika Kusini.