Habari MsetoSiasa

Serikali kuu idhibiti kisiwa cha Migingo kuzuia ghasia – Seneta

July 31st, 2019 1 min read

Na RUTH MBULA

Mizozo kuhusu umiliki wa kisiwa cha Migingo unazidi kutokota zaidi huku Seneta wa Migori Ochillo Ayacko sasa akitaka serikali ikidhibiti kuepusha wavuvi wa Kenya kushambuliwa na walinda usalama wa Uganda.

Mzozo huo ulizidi mwishoni mwa wiki wavuvi 30 wa Kenya walipokamatwa na maafisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru wa Uganda wakiwa eneobunge la Suba Kaskini na Suba Kusini Kaunti ya Homa Bay.

Bw Ayacko alisema kisiwa hicho kiko Kenya na rekodi zote za awali zimethibitisha hivyo.

Akihutubia wanahabari mjini Migori, seneta huyo alimtaka waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’I kuhakikisha amerudisha kisiwa hicho Kenya.

“Tunajua waziri ni mchapakazi na tunaamini ana uwezo wa kurudisha kisiwa chetu. Tunamuomba afanye hivyo haraka,” alisema Bw Ayacko.

Wavuvi waliokamatwa waliachiliwa baada ya kulipa faini ya Sh180,000.

Walizuiliwa katika kisiwa cha Hama nchini Uganda na walilaumiwa kwa kuingia eneo wasilopaswa na kutumia vifaa haramu vya uvuvi katika Ziwa Victoria.

Kisiwa hicho kinachozungukwa na maji ambako samaki hupatikana kwa wingi, kimekuwa kikizozaniwa na Kenya na Uganda kila nchi ikidai inakilimiki.