Habari MsetoSiasa

Serikali Kuu kuzinyima fedha kaunti 34 ambazo hazijalipa madeni

December 18th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI za kaunti 34 ambazo hazijalipa madeni yao yote halali kufikia Juni 30, 2018 huenda zikanyimwa mgao wa fedha katoka Hazina ya Kitaifa kuanzia Januari mosi 2020, kaimu waziri wa Fedha Ukur Yatani ameonya.

Kwenye taarifa iliyosomwa Jumatano na Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’I ni kaunti 13 pekee ambazo zimetii agizo ambalo alitoa mnamo Novemba 19, 2019 kwamba serikali zote za kaunti zihakikishe zimelipa madeni yote zilizokuwa zikidaiwa hadi kufikia Juni 30 mwaka jana.

“Kufikia leo kaunti ambazo zimelipa malimbikizi ya madeni yote halali kufukia Juni 2018 kama yalivyokaguliwa na kuidhinishwa na Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni 13 pekee. Kaunti hizo zinajumuisha Elgeyo Marakwet, Homa Bay, Kajiado, Kilifi, Kwale, Laikipia, Makueni, Nyamira, Nyandarua, Nyeri, Uasin Gishu, Kericho na Baringo,” akasema.

Bw Matiang’i alisoma taarifa hii nje ya afisi yake katika jumba la Harambee, Nairobi akiwa ameandamana na mawaziri wapatao 10 pamoja na mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua na Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Patrick Njoroge.

Bw Yatani alisema hatakubali sababu zozote ambazo zitatolewa na kaunti ambazo haziwalipa wanakandarasi wake na wafanyabiashara ambao waliwauzia bidhaa na huduma.

Hii ni kwa sababu Hazina ya Kitaifa imekuwa ikitoa fedha, zilizotengewa serikali za kaunti katika bajeti ya kitaifa, kwa wakati. Kwa hivyo, zile kaunti ambazo bado zinadaiwa na wanakandarasi na wawasilishaji bidhaa kufikia Juni 2018 zinahitajika kulipa madeni bila kusita,” akasema.

Miongoni mwa kaunti ambazo hazijakalimilisha kulipa madeni yao ya awali lakini yametoa mpango wa kuyalipa ni pamoja na Mombasa, Nairobi, Kirinyaga, Nakuru, Machakos na Murang’a.

Kaunti zingine ni; Taita Taveta, Turkana, Kisumu, Meru, Mandera, Kisii, Busia, Marsabit, Bungoma, Trans Nzoia, Kitui, Embu, Wajir, Lamu Bomet, Migori, Nandi, Tharaka Nithi, Vihiga, Isiolo, Tana River, Kiambu, Narok, West Pokot, Garissa, Samburu, Siaya na Kakamega inayoongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya.

Bw Yatani pia alitangaza kuwa kuanzia sasa serikali zote za kaunri zitahitajika kutoa ripoti ya kila mwezi kuhusu namna zimekuwa zikilipa madeni yote. Ripoti kama hiyo ndio itatumiwa na kama msingi wa Hazina Kuu kutuma fedha kwa serikali za kaunti..

“Kuanzia sasa kaunti zote zinashauriwa kuwa kigezo ambacho kitatumiwa kama msingi wa kutoa pesa kwa kaunti kitakuwa ni rekodi yao ya ulipaji malimbikizi ya madeni,” taarifa hiyo ikasema.

Mwezi jana Bunge la Seneti na lile la Kitaifa zilikataa ombi ya Waziri Yatani ya kutaka apewe idhini ya kuzinyima fedha kaunti ambazo hazikuwa zimelipa madeni yao kufikia Juni 30, 2018.

Kulingana na sheria sharti Waziri wa Fedha apate idhini ya mabunge yote mawili kabla ya kuzima utoaji wa fedha kwa serikali zozote za kaunti ambazo zitakiuka sheria kuhusu usimamizi wa fedha.