Serikali kuunda idara ya kufuatilia matumizi ya pesa

Serikali kuunda idara ya kufuatilia matumizi ya pesa

Na BRIAN OJAMAA

SERIKALI inanuia kuunda idara ya manunuzi katika ngazi ya kitaifa itakayohakikisha kuwa Sh500 milioni iliyotolewa kwa ajili ya ufufuaji wa kampuni ya sukari ya Nzoia imetumika ipasavyo.

Waziri wa Kilimo, Peter Munya akizungumza jana Kaunti ya Bungoma wakati wa kuzikabidhi pesa hizo kwa kampuni hiyo, alisema kila senti lazima itumike kwa kusudi lake ili kuikoa kampuni hiyo dhidi ya madeni.

“Wasimamizi wa kampuni hii imeomba ufadhili wa Sh200 milioni ili kununua mashine mpya. Tutafuatilia na kuhakikisha kuwa wamezinunua mashine hizo,” akasema Bw Munya. Alisema kamati hiyo itasaidia kumaliza ufisadi unaofilisisha kampuni hiyo.

Kadhalika, Bw Munya alisema serikali pia itatenga idadi fulani ya fedha za kuendeleza sekta ya sukari ili kupunguza madeni yanayodaiwa na sekta tofauti za kilimo. “Hatua hii itakuwa suluhisho la pekee kwa matatizo yanayokabili makampuni mbalimbali ya kilimo. Kadhalika, itashughulikia masuala ya muda mfupi kama vile kuwalipa wafanyikazi.”

Kuhusu suala la bodi ya kampuni, Bw Munya alithibitisha kwamba wanachama hao watachaguliwa hivi karibuni ili kusaidia kuangalia usimamizi. “Tutakaa na kukubaliana nani achaguliwe kuongoza usimamizi wa kampuni hii. Hatutaki kujenga picha ya upendeleo,” akasema Bw Munya.

You can share this post!

Kinda Rowe aingizwa kikosi cha Uingereza kuziba pa Rashford

Kiangazi: Wakulima hatarini kupoteza mimea

T L