Habari za Kitaifa

Serikali kuuza hisa zake katika hoteli saba

February 14th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

SIKU chache baada ya Rais William Ruto kupiga abautani na kusitisha ubinafsishaji wa kampuni tano za sukari zinazomilikiwa na serikali, Baraza la Mawaziri limeidhinisha kuuzwa kwa hisa za serikali katika mikahawa saba.

Miongoni mwa mikahawa hiyo ni pamoja na Mombasa Beach Hotel, Ngulia Safari Lodge, na Voi Safari Lodge, yote inayosimamiwa na Kenya Safari Lodges and Hotels Limited.

Mingine ni Golf Hotel Limited, Sunset Hotel Limited, Mt Elgon Lodge Limited, na Kabarnet Hotel Limited.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumatano baada ya mkutano wa Baraza la Mawaziri lililoongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi, hatua hiyo inalenga kupiga jeki ukuaji wa sekta ya hoteli nchini.

Aidha, itasaidia kuzalisha nafasi za ajira nchini.

“Kuuzwa kwa hisa za serikali katika mikahawa hii kunatarajiwa kuchochea upanuzi wa sekta ya hoteli nchini na ukuaji wa mihakawa husika kupitia uwekezaji wa sekta ya kibinafsi.

“Hatua hii inaenda sambamba na mchakato unaoendelea wa kupiga jeki sekta ya utalii kupitia mpango wa kuwaruhusu wageni kuingia Kenya bila Visa. Vile vile, hii inaendana na ahadi ya kuongeza nafasi za ajira na za kibiashara katika hoteli ambazo hisa zake zitauziwa sekta ya kibinafsi sawa na sekta yote ya utalii,” taarifa hiyo ikasema.

Majuma mawili yaliyopita Rais Ruto alibatilisha mpango wa serikali wa kubinafsisha kampuni za sukari za Nzoia, SoNy, Miwani, Muhoroni na Chemelil.

Akiongea wakati wa ziara ya siku tano katika kaunti za Bungoma na Kakamega kiongozi wa taifa badala yake aliahidi kuwa serikali yake itawekeza katika ufufuzi wa kampuni hizo zinazozongwa na madeni na changamoto nyinginezo.

“Ningependa kutangaza hapa leo (mnamo Alhamisi Februari 1, 2024) kwa kampuni ya sukari ya Nzoia na zingine za umma hazitauzwa. Hii ni mali ya wakulima na watu wa hapa na kile serikali itafanya ni kutoa pesa za kuwalipa wakulima, wafanyakazi na madeni na kulainisha utendakazi wake,” Dkt Ruto akasema kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa kampuni hiyo mjini Bungoma.

Lakini kabla ya kubadili msimamo huo, Rais alipata presha kali kutoka viongozi wa eneo hilo, wakiongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, waliopinga mpango wa serikali kubinafsisha kampuni hiyo.

Hatua ya kuuzwa kwa hisa za serikali katika mikahawa saba pia inajiri miezi minne baada ya mpango wake wa kuuza mashirika 11, ikiwemo Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta (KICC) kugonga ukuta.

Hii ni baada ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kuwasilisha kesi mahakamani kupinga hatua hiyo iliyotangazwa na Hazina ya Kitaifa mnamo Novemba 11, 2023.

Kando na KICC, mashirika mengine ambayo serikali ilipania kuuza ni pamoja na Kampuni ya Usambazaji Mafuta Nchini (KPC), Shirika la Kitaifa la Mafuta (NOC), Kampuni ya Kutengeneza Mbegu Nchini (KSC) na Kampuni ya Maziwa ya New KCC.

Mashirika mengine ni shirika la uchapishaji Kenya Literature Bureau (KLB) na Mwea Rice Mills.