Habari Mseto

Serikali kuwajali vijana wa mitaani wanaorandaranda

September 25th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI imezindua mpango wa kuwashughulikia vijana wanaorandaranda – hasa katika miji – ili kuwajali.

Mwenyekiti wa Street Families Rehabilitation Fund Bi Linah Jebii Kilimo, amesema ni vyema kuwajali vijana hao ili kuwajumuisha katika jamii.

Alitoa mwito kwa machifu kote nchini kuhakikisha wanawasajili vijana hao walio mitaani ili wajumuishwe kwenye programu ya serikali ya 4 Rs.

“Sisi sote tuna jukumu la kuwakumbatia vijana hao ili tuwalete katika jamii badala ya kuwatelekeza. Jukumu hilo lisiwe la mtu mmoja bali kila mwananchi ambaye popote pale alipo ana nafasi ya kujitolea,” alisema Bi Kilimo.

Aliyasema hayo Ijumaa wiki jana mjini Thika alipokutana na wakazi wa eneo hilo kuwahamasisha kuhusu mpango huo.

Aliwataka pia vijana hao walio mitaani washirikiane na umma popote pale walipo ili maslahi yao yaweze kushughulikiwa jinsi ipasavyo.

“Ninafahamu kuna wengine watakuwa kikwazo katika utekelezaji wa mpango huo lakini ni vyema wakishirikiana na wananchi ili waweze kupata usaidizi ufaao,” alisema Bi Kilimo.

Kisingizio

Alisema umaskini usiwe kisingizio cha kusema kuwa hiyo ndiyo maana kuna vijana hao mitaani.

Aliongeza kuwa kuna vijana wengine ambao wanatoroka makwao na kujiunga na wenzao mitaani.

Alisikitika jamii isiyojali maadili mema pia imechangia kupatikana kwa vijana wengi mitaani.

Mwenyekiti wa Street Families Rehabilitation Fund Bi Linah Jebii Kilimo. Picha/ Lawrence Ongaro

Aliwatetea walemavu akisema ni vyema pia serikali kufanya juhudi kuona ya kwamba watu hao wanapewa haki yao ipasavyo.

Alieleza kwamba walemavu wanapitia changamoto tele kama kupanda ngazi katika majumba makubwa, kuabiri matatu, kwenda katika vyoo vya umma, na hata wanapoingia katika ofisi kubwa mijini.