Serikali kuyakagua mahindi yaliyo melini kuhakikisha ni salama

Serikali kuyakagua mahindi yaliyo melini kuhakikisha ni salama

NA DAVID MWERE

SERIKALI itathibitisha usalama wa matumizi ya mahindi yaliyo kwenye meli iliyo katika bandari ya Mombasa kabla ya kusambazwa kwa Wakenya ili kuyatumia.

Hakikisho hilo lilitolewa na Halmashauri ya Kukagua Ubora wa Bidhaa Kenya (KEBS) na Mamlaka ya Kusimamia Bandari (KPA) kutokana na wasiwasi ambao umekuwepo kuwa mahindi hayo yana sumu, hivyo si salama kwa matumizi ya binadamu.

Maelezo tuliyo nayo yanaonyesha kuwa meli hiyo —MV African Merlin Voy: 01/22 —iliwasili katika Bandari ya Mombasa Novemba 21 ikiwa imebeba kiasi kisichojulikana cha mahindi yaliyotolewa kama msaada kwa Kenya kuisaidia kukabili baa la njaa.

Mahindi hayo yanadaiwa kuharibiwa na wadudu na huku yakiwa na sumu aina ya aflatoxin, hali inayoyafanya kutokuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Awali, haikuwa imebainika yalikotoka mahindi hayo, lakini afisa wa mawasiliano wa Shirika la Huduma za Ukaguzi wa Mazao Kenya (Kephis), Bi Catherine Muraguri, alisema kuwa yametoka nchini Msumbiji.

Hata hivyo, hakuthibitisha ikiwa mahindi hayo ni salama kwa matumizi ya binadamu au la.

“Kama Kephis, huwa hatushughulikii masuala ya afya ya umma. Hilo ni jukumu la idara nyingine za serikali,” akasema Bi Muraguri, huku akituelekeza katika mashirika ya Kebs na Idara ya Kusimamia Afya Bandarini (PHS). “Sisi huwa tunashughulikia wadudu na mifugo pekee,” akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Waliokosoa Ruto wapiga magoti

Raila ataja sababu za kumkabili Ruto

T L