Habari za Kitaifa

Serikali mbioni kununua silaha mpya za kisasa kukabili ongezeko la uhalifu

April 6th, 2024 1 min read

NA STEVE OTIENO

KENYA imo mbioni kununua silaha za kisasa za kivita kukabiliana na ongezeko la uhalifu nchini.

Wiki iliyopita, Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki, alizindua silaha za kisasa zenye thamani ya Sh7.6 bilioni kukabiliana na utovu wa usalama nchini.

Tayari, Rais William Ruto ameahidi kuwa ununuzi wa silaha hizo ni mwanzo tu wa mchakato wa serikali kununua zana za kisasa za kivita kukabiliana na uhalifu.

Wiki iliyopita, Rais Ruto aliongoza mkutano wa maafisa wa ngazi za juu wa usalama, ambapo aliahidi serikali itatoa ndege zaidi kwa Idara ya Polisi kuisaidia kukabilana na uhalifu.

Wizara ya Usalama wa Ndani imeagizwa kuharakisha mchakato wa kuwapa polisi silaha hizo.

Serikali imetangaza kwamba, kwa miaka mitatu ijayo, itatenga jumla ya Sh29.4 bilioni kuendesha Mpango wa Kuwapa Polisi Silaha za Kisasa (PEM).

Mpango huo unalenga kuhakikisha polisi wamepata sare, magari yaliyojihami, magari ya kuhimili vilipuzi, droni, helikopta za kuwakabili wahalifu, mashine za kuondoa vilipuzi na kadhalika.