Habari

Serikali mbioni kusaka waliotangamana na padre wa Kitui

March 30th, 2020 1 min read

NA KITAVI MUTUA

ZAIDI ya watu 50 katika Kaunti ya Kitui ambao walitangamana na padre aliyesafiri kutoka Italia wiki iliyopita na kukosa kujitenga wanasakwa na maafisa wa pilisi ili kupimwa baada ya padre huyo kupatikana na virusi vya corona.

Padre huyo wa kanisa Katoliki aliyetambuliwa kama Nicholas Maanzo, na aliyekuwa nchini Italia kwa masomo ya mwaka mmoja mjini Rome, alikimbizwa kwa kituo cha kutenga katika hospitali ya Mbagathi, Nairobi baada ya kuonyesha dalili zote za ugonjwa huo.

Jumatatu, Waziri wa Afya Bw Mutahi Kagwe alitangaza kuwa Kaunti ya Kitui ilikuwa na kisa kimoja cha ugonjwa wa corona huku idadi kamili ikigonga 50.

Alizua hofu kuu katika kijiji chake cha Kihara baada ya kukosa kujitenga, hali iliyolazimisha maafisa wa afya kuvamia nyumba yake na kumtoa.

Polisi walijulishwa na watu wa familia ya Bw Maanzo ambao walilalamika kuwa mtumishi huyo wa Mungu alifika nchini Machi 23, lakini alikuwa anaonekana kila jioni akitoka nje kabla ya siku 14 kuisha, hali iliyohatarisha maisha ya wote aliotangamana nao.

Miongoni wa wanaosakwa na polisi ili wapimwe ni wanabodaboda waliombeba, wafanyakazi wa duka kuu la Magunas aliponunua bidhaa na watu wote walioenda kutoa fedha katika mtambo wa ATM wa benki ya Absa ambapo padre huyo alitoa pesa jioni ya Machi 24.

Kulingana na afisa wa afya katika kaunti hiyo Dkt Richard Muthoka, wengine ambao watatengwa kwa lazima ni watu wa familia yake, majirani wa karibu na watawa wa kundi la Kwa-Ngindu Sisters of Good Shepherd ambapo alipitia akienda nyumbani.

Dkt Muthoka alisema makachero watatazama video za CCTV katika mtambo huo wa ATM pamoja na duka la Magunas ili kutambua watu wote waliokaribiana na padre huyo.

IMETAFSIRIWA NA FAUSTINE NGILA