Serikali na wanasiasa wajitia hamnazo njaa ikiua wakazi Marsabit

Serikali na wanasiasa wajitia hamnazo njaa ikiua wakazi Marsabit

Na NICHOLAS KOMU

HUKU kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu ujao zikinoga, wakazi wa Kaskazini mwa Kenya wanaendelea kuathirika na makali ya njaa, baadhi yao wakifariki.

Mzee Barako Elema Abudho, 69, kutoka kijiji cha Galas, eneo bunge la Horr Kaskazini, kaunti ya Marsabit ni mmoja wa walioangamia.

Kwa wiki kadha, mzee huyo aliishi bila chakula, akitegemea maji kidogo kutoka kwa majirani zake.

Wakazi wa kijiji hicho hawangemudu gharama ya chakula cha kumwezesha mzee huyu kuendelea kuishi.

Aidha, hawangemudu gharama ya chakula cha kukidhi familia zao.

Katika kijiji kingine cha Ileret, Bi Aigus Nyemeto anawatuliza watoto wake wanane ili walale. Hii ni siku ya nne kwa familia ya mama huyo, ambaye ni mja mzito, kulala bila chakula.

Watoto hao wanaonekana wachovu baada ya kuathirika na utapiaji mlo.

Mumewe Aigus huwa haji nyumbani baada ya familia hiyo kupoteza mifugo yao 360 kutokana na makali ya kiangazi.

“Mume wangu hajafika nyumbani tangu mifugo yetu ilipofariki. Anahisi hana chochote alichobaki nacho kuipa familia yake,” akasema.

Kufikia sasa mama huyo anataraji kuwa muujiza utatendeka wapate chakula, au wahisani wawape misaada ya chakula.

Umbali wa kilomita 100 kutoka Manyatta ya mama Aigus maisha ya mzee Duba Kanchoro, 90, yamo hatarini.

Ameishi kwa maji na chai kwa siku kadha lakini mwili wake unaendelea kudhoofika kwa kukosa chakula.

Hulala kwenye ngozi ya ng’ombe akisubiri chakula au kifo.

Baada ya Kaunti ya Marsabit kukosa mvua kwa zaidi ya miaka miwili, mamia ya wakazi wamekuwa wakisakamwa na njaa.

Wakazi wanalazimika kutembea umbali wa mamia ya kilomita huku wengine wakipoteza matumaini maishani.

Maelfu ya watoto wamelazimika kuacha shule kwa kukosa chakula shuleni na nyumbani.

Mamia ya mifugo inakufa kila siku.

Godana Boru alazimika kulisha mifugo yake karatasi kwa kukosa malisho katika eneo la Horri Guda, Horr Kaskazini, Kaunti ya Marsabit. Kiangazi kikubwa kilichosababishwa na ukosefu wa mvua kwa miaka miwili kimehangaisha zaidi ya familia 160,000 huku maelfu ya mifugo pia ikiangamia. Wakazi wanalilia wahisani na serikali kupeleka msaada wa dharura. PICHA | NICHOLAS KOMU

Katika Kaunti ya Marsabit pekee, jumla ya familia 160,000 zinakabiliwa na baa la njaa huku idadi hiyo ikitarajiwa kupanda hadi 200,000 katika wiki zijazo.

Lakini serikali haijachukua hatua zozote kuwaondolea wakazi wa Marsabit madhila.

Hii ni licha ya Rais Uhuru Kenyatta, mnamo Septemba 2021, kutangaza ukame kuwa janga la kitaifa.

Aidha, wanasiasa wanaogombea urais pia hawajachukua hatua zozote za kutoa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa eneo hili. Hii ni licha ya kwamba wanasiasa hao wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, kutoa ahadi nyingi wanazodai zitaboresha maisha ya Wakenya.

Miezi mitano baada ya Rais Kenyatta kutangaza ukame kuwa janga la kitaifa, wanasiasa hawa, mashirika ya kibinafsi hayajatoa misaada yoyote kwa wakazi wa Marsabit.

“Hali ni mbaya. Hiki ni kiangazi kibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini ndani ya miongo kadha iliyopita. Tumepokea ripoti kwamba mtu mmoja amekufa. Watu wengine kadha huzirai kwa kulemewa na njaa,” akasema Wario Guyo, ambaye ni mkurugenzi wa Shirika la kutoa misaada kwa jamii za wafugaji, Pastoralist Community Initiative and Development Assistance (PACIDA).

Mashirika ambayo hutoa misaada ya chakula na maji katika maeneo hayo sasa yanaomba wahisani kupeleka misaada ya dharura kwa wakazi wa Marsabit.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Serikali imezembea kufanikisha...

Ruto apasua OKA

T L