Habari Mseto

Serikali sasa huru kuorodhesha MRC kundi la kigaidi

September 9th, 2020 1 min read

Na PHILIP MUYANGA

SERIKALI sasa iko huru kuendeleza mipango ya kuliorodhesha kundi la Mombasa Republican Council (MRC) kama la kihalifu na kigaidi.

Hii ni baada ya mahakama kuu ya Mombasa kutupa nje kesi ambapo viongozi watatu wa MRC walikuwa wamepinga notisi ya Inspekta Jenerali wa polisi iliyotaka waeleze kwa nini kundi hilo lisiorodheshwe jinsi hiyo.

Jaji Eric Ogola alitupilia mbali kesi hiyo iliyokuwa imewasilishwa na kiongozi wa MRC Bw Omar Mwamnuadzi, Bw Randu Nzai na Abdallah Ali miaka mitano iliyopita akisema kuwa haikuwa na msingi wowote.

Mahakama ilisema wanachama wa MRC waliweka wazi nia yao ya kujitenga na Kenya na pia wanakumbwa na madai ya kutekeleza mashambulizi katika maeneo yenye usalama.

Iliamuliwa kwamba Inspekta Jenerali wa polisi alikuwa na haki kutoa notisi hiyo iliyotoa saa 24 kwa MRC kujitetea.

“Wakati huo wa saa 24 uliopeanwa kwa walalamishi kujibu notisi hiyo ni sawa ikitiliwa maanani hali kuhusiana na kundi hilo,” alisema Jaji Ogola.