Habari Mseto

Serikali sasa kufuatilia mawasiliano ya WhatsApp

November 2nd, 2018 1 min read

Na PATRICK ALUSHULA

Serikali inatathmini kudhibiti matumizi ya WhatsApp na Skype katika hatua ambayo inaweza kulazimisha wamiliki wa huduma hizo kutoa habari kwa serikali.

Mamlaka ya Mawasiliano (CA) inatafuta mwanakandarasi wa kuchunguza na kuamua jinsi huduma hizo zinaweza kudhibitiwa.

Mamlaka hiyo inataka kuwa na uwezo wa kudhibiti kama inavyofanya mawasiliano ya simu ya kampuni za mawasiliano ya kawaida (pasi kutumia intaneti).

WhatsApp ni huduma ya mawasiliano ambayo imesimamiwa na Facebook na hutumia intaneti.

“Tunataka kuchukua hatua hiyo kutokana na ukweli kwamba wamiliki wa huduma hizo wanaweza kuwa na habari kuhusu wateja na hawana afisi humu,” ilisema CA katika taarifa.

Mamlaka hiyo itatathmini matokeo na mapendekezo ya mshauri na kuamua kuhusiana na masuala ambayo yatatekelezwa katika wajibu wake wa kusimamia mawasiliano.

Chini ya kanuni za CA, wamiliki wa huduma kama WhatsApp na Skype watatakiwa kutimiza “masharti ya usalama na usiri,” kama inavyohitajika kisheria.

Sheria hizo pia zitajumuishwa kuhusiana na jinsi huduma hizo zitatolewa kuambatana na mahitaji ya mashirika ya usalama kuhusiana na utoaji wa data kama zinavyofanya kampuni kama vile Safaricom inapoagizwa na mahakama.

Kwa sasa, matumizi ya huduma hizo hayajasimamiwa na sheria yoyote.

CA inapendekeza hilo wakati ambapo wadhibiti ulimwenguni wanataka kuwa na kiwango fulani cha kudhibiti sekta hiyo.