Habari

Serikali sasa yaahirisha kufunguliwa kwa shule

August 10th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

WANAFUNZI sasa watarejea shuleni Septemba 2, baada ya Wizara ya Elimu kuongeza likizo yao kwa wiki moja ili kutoa nafasi kwa Sensa ya Kitaifa.

Shule za msingi na upili za umma zilikuwa zimeratibiwa kufunguliwa Agosti 26.

Kulingana na taarifa kutoka kwa wizara hiyo Ijumaa, hatua hiyo ilifikiwa baada ya siku za sensa hiyo kulingiliana na wakati shule zingefunguliwa.

Sensa hiyo imepangiwa kufanyika kuanzia usiku wa Agosti 24 hadi 25. Kutokana na hayo, Muhula wa tatu utaanza Septemba 2 na kuisha Oktoba 2.

Kwenye agizo hilo, Katibu wa Elimu Bellio Kipsang alisema hatua hiyo itawawezesha wale watakaoendesha shughuli hiyo kumhesabu kila mmoja bila matatizo yoyote.

“Kwa shughuli hiyo kufanikiwa, ni lengo kuu la Halmashauri ya Kitaifa Kuhusu Takwimu (KNBS) kuwa hakutakuwa na watu wengi wanaosafiri ili kuwawezesha kuwahesabu watu wengi zaidi iwezekanavyo. Hilo litahakikisha wanafunzi wamehesabiwa,” akasema Dkt Kipsang.

Halmashauri hiyo ilisema itatumia mitambo ya kidijitali kuendesha shughuli hiyo, ili kuhakikisha maelezo muhimu kuhusu Wakenya wote yamenakiliwa.

Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri hiyo Bw Zachary Mwangi alisema, hatua hiyo inalenga kuhakikisha hakutakuwa na malalamishi yoyote, kama ilivyokuwa kwenye Sensa ya 2009.

“Tuna imani kuwa mashine tutakazotumia ni mahsusi, kwani tumezifanyia majaribio kadhaa,” akasema Bw Mwangi.

Maafisa wapata mafunzo

Vilevile, alisema maafisa watakaoendesha shughuli hiyo wamepata mafunzo ya kutosha.

“Wamekuwa wakipokea mafunzo maalum kuhusu mfumo wa kuhesabu watu wa kidijitali tangu Aprili,” akasema.

Wakenya pia watatoa maelezo kuhusu kilimo chao; ikiwa wanaendesha ukulima wa kawaida ama ufugaji samaki.

Kinyume na sensa zingine, kila familia pia itahitajika kueleza ikiwa inamiliki mifugo wa kisasa ama wa kiasili kama ng’ombe, kondoo, mbuzi, punda kati ya wengine.

Maelezo kuhusu mimea yataangazia ikiwa familia husika inakuza majanichai, kahawa, maembe kati ya mimea mingine ya kibiashara.

Halmahauri hiyo ilisema maelezo hayo yatatumika kwenye tafiti mbalimbali kuhusu hali ya kilimo nchini.