Habari Mseto

Serikali sasa yaongeza muda wa raia kupata paspoti mpya

July 25th, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta ameagiza muda wa kutoa paspoti mpya ya kielektroniki iongezwe hadi Machi 2020.

Idadi kubwa ya Wakenya nchini na wanaoishi mataifa ya nje, walikuwa wamelalamika kwamba hawangeweza kubadilisha paspoti zao kufikia Agosti 31, mwaka huu ambao ndio ulikuwa ni muda wa mwisho kupata hati hiyo mpya.

Msemaji wa Serikali, Kanali Mstaafu Cyrus Oguna jana alisema kufuatia agizo hilo la Rais, Wakenya watakuwa huru kuendelea kutumia paspoti walizo nazo hadi Machi 1, 2020.

Kulingana naye, Rais Kenyatta aliagiza Mawaziri Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani na Uratibu wa Serikali Kuu) na Bi Monica Juma (Mashauri ya Kigeni) washirikiane na afisi zote za ubalozi za Kenya zilizo nchi za kigeni, ili wananchi waendelee kupewa Visa za kimataifa bila kutatizwa wakitumia paspoti za kawaida.

“Usajili wa paspoti mpya utaendelea kitaifa na Wakenya wanaombwa watumie muda ulioongezwa vyema, wasisubiri hadi dakika za mwisho kujisajili,” akasema Bw Oguna, kwenye taarifa kwa vyumba vya habari.

Wakenya walio katika nchi za kigeni ambao walizungumza na Taifa Leo jana walisifu hatua hiyo kwa vile sasa wana muda kujiandaa vyema.

Katika Kaunti ya Nairobi, ilikuwa ikiwalazimu wananchi kuwasili katika afisi ya usajili wa paspoti hata saa tisa usiku ili wapate nafasi mapema.

Wakenya wanaoishi ng’ambo walikuwa wameeleza mahangaiko yao kutafuta paspoti hizo mpya kwani hazipatikani katika kila nchi.

Baadhi ya waliohamia nchi jirani kama vile Uganda na Tanzania, walikuwa wangali wanawazia hatimia yao ifikapo Agosti 31, kwani wanahitaji kugharamia usafiri wa familia zao nzima kuja Kenya kutafuta paspoti mpya. Serikali iliamua kuongeza afisi za usajili wa paspoti katika maeneo mbalimbali nchini.