Habari Mseto

Serikali sasa yaruhusu wavuvi kutumia nyavu zilizokataliwa

August 13th, 2018 2 min read

Na CHARLES LWANGA

SERIKALI sasa imeruhusu wavuvi katika bahari ya Hindi kutumia nyavu ambazo awali zilikataliwa, kwa kuwa zinavua hadi samaki wachanga.

Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya wadau katika sekta ya uvuvi kupiga kura na kuamua neti hizo zilizokuwa zimepigwa marufuku sehemu nyingi za bahari ya Hindi, zinaweza kutumiwa kuvua samaki.

Uamuzi huo uliafikiwa wakati wa mkutano wa kutatua mgogoro wa wavuvi uliohudhuriwa na maafisa wakuu wa Kaunti ya Kilifi, wanajeshi na maafisa wa wanyamapori pamoja na wavuvi na wachuuzi wa samaki.

Wakati huo huo, Naibu mkurugenzi wa Uvuvi eneo la Pwani, Bw Collins Kambu Ndoro, alitoa mwelekeo jinsi nyavu hizo tata zinafaa kutumiwa na kuonya kuwa watakaoenda kinyume na mwelekeo huo watachukuliwa hatua kali.

Akizungumza na wadau baada ya mkutano, Bw Ndoro alisema nyavu hizo zitatumiwa ndani ya maji makuu na samaki watakuwa wanavuliwa kwa mashua.

“Wavu huo utakuwa unatumika kuanzia Oktoba hadi Machi na wale wote watakaopatikana wakitumia wavu huo kuvua samaki nje ya msimu huo watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.

Hata hivyo, baadhi ya washikadau, wakiwemo wavuvi na wachuuzi wa samaki walipokea hatua hiyo kwa furaha wakisema kuna mahitaji mengi ya samaki sokoni haswa msimu huu ambao hoteli nyingi zinajiandaa kupokea watalii.

“Samaki wakiwa wengi sokoni fursa hiyo itaajiri vijana wengi na kupunguza visa vya ujambazi maeneo haya,” alisema Bw Khamis Mohamed, ambaye ni mvuvi eneo la Watamu.

Licha ya hayo, baadhi ya wavuvi walipinga vikali matumizi wa wavu huo wakisema huenda ukavua samaki wachanga na kuangamiza samaki maeneo ya Malindi. Mchuuzi wa samaki Bi Zawadi Karisa, alisema kuwa wavuvi wanaotumia wavu huo spesheli huwa ndio wanaowauzia samaki bila ubaguzi.

“Baadhi ya wavuvi hubagua wanao wauzia samaki na ni vyema serikali kupitisha hoja hii inayowaruhusu wavuvi wanaoenda maji makuu kuvua samaki,” alisema na kuongeza kuwa “hatua hii itapunguza uhaba wa samaki na kuwalazimisha wavuvi watuuzie samaki bila ubaguzi.”