Michezo

Serikali Ujerumani yaruhusu kipute cha Bundesliga kirejelewe Mei 15

May 7th, 2020 2 min read

CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA

CHANSELA wa Ujerumani, Angela Merkel, amethibitisha kwamba upo uwezekano mkubwa kwa Ligi Kuu ya taifa hilo (Bundesliga) kurejelewa mwezi huu wa Mei.

Kutimia kwa hilo kutafanya Bundesliga kuwa ya kwanza miongoni mwa Ligi Kuu za bara Ulaya kuanza upya baada ya shughuli za michezo muhula huu kuvurugwa na corona.

Waendeshaji wa kivumbi hicho (DFL) wametoa mpangilio utakaofuatwa na tarehe kamili ya kurejelewa kwa kampeni za gozi hilo.

Mechi zote zilizosalia katika kalenda ya Bundesliga msimu huu zitasakatiwa ndani ya viwanja vitupu bila mashabiki.

Zikisalia mechi tisa pekee kwa muhula huu kutamatika rasmi, Bayern Munich ambao ni mabingwa watetezi wa Bundesliga wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama nne zaidi kuliko Borussia Dortmund.

Mwenyekiti wa Bayern, Karl Heinz Rummenigge amesema, “Ningependa kuwashukuru wanasiasa kwa maamuzi yao ya kihistoria ambao yanatoa fursa kwa kivumbi cha Bundesliga kukamilishwa msimu huu.”

“Kwa sasa tunatazamia kurejelea ligi wakati wowote kuanzia katikati ya Mei 2020. Hii itahakikisha kwamba maamuzi yote mengine katika sekta ya michezo yatafanyika uwanjani,” akasema.

“Namsihi kila mmoja anayehusika kuzingatia kanuni zote ambazo zimetolewa na serikali kwa kuwa ndio msingi wa kurejelewa kwa Bundesliga. Nidhamu ya hali juu miongoni mwa washikdau ni ushindi kwa Wajerumani na ulimwengu mzima katika juhudi za kukabiliana na janga la corona,” akaongeza kinara huyo.

Kwa upande wake, Christian Seifert ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa DFL alisema, “Maamuzi ya leo ni habari njema kwa vipute vya Bundesliga na Ligi ya Daraja la Kwanza (Bundesliga 2). Ni hatua ambayo imetegemezwa kwa nidhamu ya hali ya juu kutoka kwa klabu husika na waajiriwa wao ambao wanatazamiwa kutekeleza sheria za afya zilizopo.”

“Michuano bila mashabiki si suluhu kwa yeyote. Ingawa hivyo, huenda ikawa ndiyo njia ya pekee ya kudumisha hadhi ya ligi za Ujerumani msimu huu,” akaongeza.

Tangazo la Merkel kwa pamoja na vinara wa soka ya Ujerumani linatolewa siku moja baada ya wachezaji 10 wa klabu za Bundesliga na Bundesliga 2 kupatikana na virusi vya corona kufuatia vipimo ambavyo watu 1,724 walifanyiwa nchini Ujerumani.

Awali, DFL ilikuwa imeonya kwamba hali ya kifedha miongoni mwa klabu mbalimbali za soka ya Ujerumani ingekuwa mbaya zaidi iwapo kampeni za msimu huu zisingerejelewa kufikia Juni 2020.

Wachezaji wengi wa Bundesliga walirejea kambini mwezi jana baada ya DFL kudokeza uwezekano wa kuanza upya kwa kipute hicho mnamo Mei 9.

Hafla zote zinazohusisha mikusanyiko mikubwa ya watu imepigwa marufuku nchini Ujerumani hadi Oktoba 24. Ingawa Serikali imependekeza mechi zote kuchezewa ndani ya viwanja vitupu, DFL inashirikiana na maafisa wa afya na wa usalama kutathmini uwezekano wa takriban mashabiki 300 pekee kuruhusiwa kuingia uwanjani kushangilia wachezaji wa vikosi vyao.

Kwa mujibu wa takwima, chini ya watu 7,000 ndio wameaga dunia nchini Ujerumani kutokana na virusi vya corona.

Idadi hii ndiyo ndogo zaidi ikilinganishwa na mataifa mengine ya bara Ulaya, hususan Uingereza, Italia, Ufaransa na Uhispania.