Serikali ya Israel yapiga jeki mpango wa utekelezaji 4-K Club kupitia mchango wa miche ya mboga

Serikali ya Israel yapiga jeki mpango wa utekelezaji 4-K Club kupitia mchango wa miche ya mboga

Na SAMMY WAWERU

UFUFUZI wa mpango wa 4-K Club katika shule nchini umepigwa jeki baada ya serikali ya Israel kutoa msaada wa miche 10,000.

Kupitia ubalozi wa taifa hilo nchini, Israel imetoa mchango wa miche 5,000 ya sukumawiki na kiwango sawa na hicho cha spinachi.

Miche hiyo imesambazwa kwa shule 10 katika Kaunti ya Nairobi.

Akiahidi kusaidia kuendeleza mpango wa 4-K Club, Waziri wa Kilimo Peter Munya alisema uteuzi wa shule zitakazonufainika na miche hiyo ulizingatia nafasi ya ardhi na uwezo kuitunza.

4-K Club ikilenga kusaidia kuboresha sekta ya kilimo nchini, Bw Munya alisema uzinduzi wake utakuwa wenye manufaa makubwa kufanikisha mojawapo ya Ajenda Nne Kuu za Rais, kuwepo kwa chakula cha kutosha na usalama.

Juni 4, 2021, Rais Uhuru Kenyatta alizindua upya mpango huo, kuanza kutekelezwa katika shule zote za msingi na upili nchini.

“Wizara yangu itaendelea kupiga jeki 4-K Club, mpango ambao unalenga kukuza wanafunzi katika sekta ya kilimo na ufugaji. Ufuufuzi wake unaenda sambamba na Ajenda ya Rais kuhakikisha nchi hii ina chakula cha kutosha na salama,” Bw Munya akasema wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa miche hiyo kwa shule zitakazonufaika.

Waziri alisema ufufuzi wa mpango wa 4-K Club kando na kunoa wanafunzi, pia unapania kushirikisha na kuandaa kizazi kijacho cha vijana kufanikisha sekta ya kilimo.

Alisema wizara yake kwa ushirikiano na ile ya maji, inafanya mipango kuhakikisha kila shule ina chanzo cha maji ya kutosha, kama vile kuchimba mashimo na mabwawa.

“Shule pia zikumbatie mfumo wa uvunaji maji ya mvua ili tuendeleze mpango huu,” Bw Munya akahimiza.

“Kwa vijana walio kwenye kilimo, mkumbatie matumizi ya teknolojia ya kisasa kukiboresha. Muwe wabunifu katika nyanja mbalimbali za kilimo,” waziri akashauri.

Akizungumza wakati wa usambazaji wa miche hiyo Kilimo House, Nairobi, Balozi wa Israel nchini Kenya Oded Joseph, alipongeza jitihada za Rais kufufua 4-K Club, akieleza kwamba itasaidia kuimarisha sekta ya kilimo.

“Huu ni mwanya wa kipekee kushirikisha vijana katika nyanja ya uzalishaji wa chakula, usambazaji na pia uongezaji thamani. Utasaidia kuangazia uhaba wa chakula, waukumbatie,” balozi akahimiza.

Aidha, Bw Oded aliahidi mchango wa serikali ya Israel katika kusaidia kufanikisha 4-K Club.

Huku kiwango cha fedha kilichotumika kuufufua kikiwa hakijabainika, Wizara ya Kilimo inasema inaendelea kupokea mchango kutoka kwa wadauhusika mbalimbali.

Wizara hiyo inasisitiza kwamba ina mpango faafu kufanikisha 4-K Club.

Kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu, Waziri Msaidizi (CAS) katika Wizara ya Kilimo, Anne Nyaga alisema wanalenga kuhami walimu ili kuuendeleza.

“Tumezindua kamati ya vijana katika kiwango cha wizara, kutoka vitengo mbalimbali ambao jukumu lao ni kutoa mwelekeo, mikakati na maagizo faafu,” Bi Nyaga akafafanua.

Alisema Wizara ya Kilimo inashirikiana na wizara nyinginezo tano.

“Kamati hiyo ya vijana pia inatathmini utendakazi wa vijana wengine nchini kwenye kilimo na kutoa mwelekeo,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Mfanyakazi wa hoteli akana kuwahadaa wafanyabiashara...

Shevchenko aacha kazi ya ukocha katika timu ya taifa ya...