Habari

Serikali ya kaunti yafuta bili za waliovamiwa na genge Mombasa

August 7th, 2019 1 min read

Na MISHI GONGO

NAIBU Gavana wa Kaunti ya Mombasa Dkt William Kingi amesema serikali ya kaunti imefutilia mbali bili za hospitali za wote ambao walifikishwa katika hospitali kuu ya Pwani kupewa matibabu baada ya kuumizwa na genge.

Genge la Wakali Kwanza linashukiwa kuhusika.

Akizungumza Jumanne katika hospitali hiyo alipowatembelea majeruhi, Dkt William Kingi alisema kaunti itahakikisha kuwa wanapokea matibabu bora bila kutozwa ada yoyote.

Wakati huo huo aliwaomba wakazi wenye habari zozote zitakazosaidia kukamatwa kwa waliyotekeleza unyama huo kupiga ripoti mara moja kwa polisi bila woga.

Aidha aliwaomba maafisa wa polisi kuharakisha uchunguzi ili kuwatia mbaroni wahalifu hao, akisema kuwa huru kwao kutasambaratisha sekta ya utalii nchini.

“Waliyotekeleza mashambuliyo haya ni jamaa zetu, wanaishi miongoni mwetu na hivyo tuwasalimishe kwa polisi ili kusaidia kudumisha amani katika mitaa yetu,” alisema Bw Kingi.

Mkurugenzi mkuu wa mradi wa Inua Mama Mashinani mjini Mombasa, Bi Gladys Chepkorir ambaye pia alikuwa ameenda kuwafariji jamaa za majeruhi aliwaomba wazazi na wenyeji katika mtaa wa Kisauni kuwa katika mstari wa mbele kudumisha amani kwani ni jukumu lao pia.

Kurekebisha mienendo

Aidha, aliwaomba wazazi wa genge hilo kuwasalimisha watoto wao kwa serikali ili wapate mafunzo yatakayosaidia kurekebisha mienendo yao.

“Wazazi kuwaweka watoto hawa majumbani ni kuwaharibu zaidi, unaponyamaza unajiweka katika hatari ya kuvamiwa wewe siku zijazo,” alisema.

Mmoja wa waathiriwa ambaye alivamiwa akiwa katika biashara yake ya bodaboda, Bw Julius Katana ameeleza kuwa alinusurika kupoteza mkono wake wa kulia katika shambulio hilo.

Alisema wahalifu hao walisimamisha pikipiki yake kisha kuanza kumshambulia kwa mapanga.

Bw Julius alifanyiwa upasuaji ili kuunganishwa mkono huo.

Watu si chini ya 11 walipata majeraha mabaya katika shambulio hilo, sita kati yao tayari wamesharuhusiwa kuenda nyumbani huku watano wakiwa wangali wanapokea matibabu.