Habari Mseto

Serikali ya Kenya ilihadaa mahakama – Miguna Miguna

February 22nd, 2018 1 min read

Bw Miguna Miguna alipofikishwa katika mahakama ya Kajiado Februari 6, 2018. Picha/ KANYIRI WAHITO
Bw Miguna Miguna alipofikishwa katika mahakama ya Kajiado Februari 6, 2018. Picha/ KANYIRI WAHITO

Na BENSON MATHEKA

WAKILI Miguna Miguna, sasa anadai kwamba serikali ya Kenya ilidanganya mahakama kuhusu paspoti yake iliyotwaliwa kabla ya kufurushwa Kenya.

Bw Miguna alisema serikali kupitia idara ya uhamiaji, haikutii agizo la mahakama la kuwasilisha paspoti hiyo kortini mbali ilichofanya ni kuwasilisha paspoti feki.

Mnamo Jumatano, mkurugenzi wa uhamiaji, Bw Gordon Kihalangwa, kupitia kampuni ya mawakili ya Ngatia and Associates, aliwasilisha paspoti ya Kenya ya Bw Miguna alivyoagizwa na Jaji Luka Kimaru wiki tatu zilizopita ikiwa imeharibiwa.

Bw Kihalangwa alisema ni kawaida ya paspoti kuharibiwa watu wanazozimiliki wakitimuliwa nchini na kwamba kufurushwa kwa wakili huyo kulikuwa halali.

Hata hivyo, Bw Miguna alisema Bw Kihalangwa alikaidi agizo la Jaji Kimaru la kuwasilisha paspoti yake halali katika muda wa siku saba baada ya agizo kutolewa.

“Washtakiwa hawakutii agizo la Jaji Kimaru. Agizo la Mahakama linaeleza wazi kwamba washtakiwa ni lazima wawasilishe paspoti kwa msajili wa Mahakama Kuu katika muda wa siku saba,” alisema Bw Miguna.

Aliendelea: “Hii inamaanisha kuwa kurudishwa kwa paspoti halali, inayotumika ilivyokuwa walipoitwaa kwa nguvu na kinyume cha sheria kutoka kwangu.”

Kulingana na Bw Miguna, washtakiwa hawakuagizwa kuwasilisha mahakamani paspoti tofauti na walichompokonya.

 

Kukaidi agizo

“Kile ambacho serikali hii haramu imefanya ni kuwasilisha paspoti iliyoharibiwa kwa kukaidi agizo la korti,” alisema.

Alisema Bw Kihalangwa alidanganya mahakama kwamba aliasi uraia wake Kenya 1986 ikidai mwaka huo alikuwa katika chuo cha Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS) kilichoko Gilgil.

“Kihalangwa sasa anadai kwamba nilipoteza uraia wangu 1986. Kutoka Februari hadi Agosti nilikuwa chuo cha NYS, Gilgil. Kutoka Septemba hadi Desemba 1986 nilikuwa mwanafunzi @uonbi, chuo kikuu cha Nairobi) Kenya,” alisema.

Alisema kuanzia Machi 2 , ataanza ziara ulimwenguni itakayong’oa nanga  Washington, Amerika katika kampeni aliyoitaja kama “vita vikuu vya ukombozi.”