Serikali ya Kenya yakosolewa kwa kupuuza sekta ya ufugaji

Serikali ya Kenya yakosolewa kwa kupuuza sekta ya ufugaji

NA SAMMY WAWERU

SERIKALI ya Kenya imeshauriwa kuipa kipau mbele sekta ya ufugaji kufuatia mchango wake mkuu katika uboreshaji uchumi.

Mwanauchumi anayeshughulikia masuala ya mifugo katika Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Ugo Pica-Ciamarra amesema sekta ya ufugaji ikitiliwa maanani itasaidia kwa kiasi kikubwa kuangazia kero ya ukosefu wa kazi hasa miongoni mwa vijana.

Wadauhusika katika sekta hiyo, wamekuwa wakilalamikia mgao finyu unaotolewa wakati wa ugavi wa fedha za serikali ya kitaifa – makadirio ya bajeti.

“Ufugaji ni mojawapo ya sekta ambazo zikitiliwa maanani, itainua uchumi pakubwa. Serikali ya Kenya ikaze kamba hususan katika ugavi wa fedha,” Bw Ugo akaambia Taifa Leo, kupitia mahojiano ya kipekee.

Afisa huyo aidha alisema nchi zilizoboresha huduma za ufugaji, ni kutokana na hatua ya serikali kushika mkono wafugaji na kufanya mazingira ya utendakazi kuwa bora.

Nyuzilandi, Amerika, Ujerumani, Ufaransa, Australia na Ayalandi ni kati ya mataifa bora ulimwenguni yaliyoimarisha huduma za ufugaji, hususan ng’ombe wa maziwa.

“Wanachohitaji wakulima na wafugaji ni mkono wa serikali, kushusha bei ya bidhaa za mifugo na kulainisha miundomsingi ya soko,” mtaalamu huyo akahimiza.

Kauli ya Bw Ugo imejiri wakati ambapo bei ya chakula cha mifugo inaendelea kuwa ghali.

Wafugaji wanalalamikia mfumko wa bei ya chakula cha madukani, Ugo akiishauri serikali kuzindua mpango wa malisho ya bei nafuu.

Sekta ya kuku imeathirika kwa kiasi kikuu, baadhi wakilazimika kuacha shughuli ya ufugaji-biashara.

Mahangaiko yanayozingira wakulima, yamechangia kuwa na uhaba wa maziwa hatua ambayo imesababisha bidhaa hiyo kuwa ghali.

Mfugaji wa ng’ombe wa maziwa. Serikali imeshauriwa kutilia maanani sekta ya ufugaji. PICHA | SAMMY WAWERU

Kwa sasa, pakiti ya mililita 500 inachezea kati ya Sh58 – Sh70.

Gharama ya ufugaji Kenya haikamatiki, licha ya kuwa ongezeko la malighafi ya bidhaa za mifugo ni changamoto ya kimataifa haswa baada ya janga la corona kutokea 2020.

Wafugaji maeneo kame wanakadiria hasara ya mifugo wao kufa njaa na wengine kusombwa na mafuriko.

“Nimepoteza mifugo wenye thamani ya Dola 9, 800 (sawa na Sh980,000 pesa za Kenya), kupitia ukame na mafuriko,” anasema Tumal Galdibe, mfugaji katika Kaunti ya Marsabit.

Galdibe analalamikia jinsi serikali inavyojikokota kuangazia changamoto zinazozingira jamii za wafugaji.

“Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) yanajaribu kutuletea afueni, ila serikali imezembea. Inatoa suluhu ikiwa Nairobi. Mapendekezo yanayotolewa maeneo ya mijini ni vigumu kufikia waathiriwa – jamii za wafugaji maeneo kame,” Galdibe alia, akihimiza serikali kubadilisha mifumo yake ya sheria kuangazia majanga.

Maeneo kame yanategemewa pakubwa katika uzalishaji wa nyama nchini.

  • Tags

You can share this post!

Wagombea urais 55 wahatarisha uchaguzi

Dereva Kimathi amaliza nambari nne mkondo wa sita mbio za...

T L