Serikali ya Lamu lawamani kwa kulipa wafanyakazi hewa wapatao 112

Serikali ya Lamu lawamani kwa kulipa wafanyakazi hewa wapatao 112

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imelaumiwa kwa kutumia mamilioni ya fedha kila mwezi kulipa mishahara ya wafanyakazi zaidi ya 100 ambao hawajulikani waliko.

Haya yalifichuka wakati wa hafla ya kukabidhi ripoti ya ukaguzi wa wafanyakazi wa kaunti iliyoandaliwa na Bodi ya Kuajiri Wafanyakazi katika Kaunti (PSB).

Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kuzindua ripoti hiyo, Mwenyekiti wa PSB katika Kaunti ya Lamu, Bw Abdallah Fadhil, alisema majina 112 ya wafanyakazi ambao hawapo yalitambuliwa baada ya kukosa kujitokeza ili kukaguliwa na bodi.

Kwa kipindi cha miezi mitatu, PSB ilifaulu kutekeleza ukaguzi na uhakikishaji wa wafanyakazi 1,693 wanaohudumia idara mbalimbali za Serikali ya Kaunti ya Lamu kabla ya kuandaa ripoti hiyo.

Bw Fadhil alisema PSB tayari imewatwika majukumu maafisa wakuu wa idara kufanya uchunguzi wao wa kina na pia kuwasilisha ripoti zao kuhusiana na kuwepo kwa wafanyakazi hao ghushi.

Aidha, alisema PSB tayari imetoa pendekezo la kusimamishwa kwa mishahara ya kila mwezi ya wafanyakazi hao hadi pale idara husika zitakapotoa ripoti kuwahusu na iwapo wengine watapatikana kuwepo kwa njia moja au nyingine.

“Baada ya miezi mitatu ya kukagua watendakazi wa serikali ya kaunti ya Lamu, tulipata kunao wafanyakazi hewa 112 wanaopokea mishahara lakini hawapo. PSB ilijaribu kuwatafuta ili kushiriki ukaguzi lakini hawakupatikana,” akasema Bw Fadhil.

Ripoti hiyo pia ilifichua kwamba Serikali ya Kaunti ya Lamu imeajiri watu 25 pekee walio na ulemavu, ambao wanawakilisha asilimia 1.5 pekee ya jumla ya wafanyakazi wote wa serikali ya kaunti hiyo.

Jinsia kwenye uajiri wa wafanyakazi wa serikali ya kaunti ya Lamu pia iliwakilishwa na asilimia 59 ya wanaume na 41 ya wanawake.

Uwakilishi wa vijana katika nafasi za ajira serikali ya kaunti hiyo ni asilimia 48.2.

Uwakilishi

Ripoti hiyo pia ilifichua kuwa makabila asili ya Lamu yanawakilishwa na asilimia 67 ya wafanyakazi walioko kwenye serikali ya kaunti ilhali watu wa makabila madogo wakiwakilishwa kwa asilimia 1.5 pekee.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo kwa niaba ya Gavana wa Lamu, Fahim Twaha, Waziri wa Fedha wa Lamu, Bw Abdu Godana, alisema ukaguzi uliofanywa utasaidia serikali ya kaunti ya Lamu kufuatilia utendakazi na kujukumika kwa wafanyakazi wake.

“Nafurahi kwamba ripoti imeonyesha wazi jinsi kaunti ya Lamu ilizingatia makabila na jinsia zote katika kuajiri wafanyakazi bila mapendeleo. Ripoti pia itasaidia kuhakikisha kuna uwazi na uwajibikaji miongoni mwa wafanyakazi na idara husika,” akasema Bw Godana.

Ilibainika kuwa, idara ya afya katika kaunti ndiyo imeajiri idadi kubwa zaidi ya wafanyakazi katika kaunti ikifuatwa na idara ya usimamizi wa huduma za umma.

Idara zilizo na idadi ndogo zaidi ya wafnayakazi ni ile ya masuala ya vijana, na idara ya utalii.

Serikali ya kaunti ilishauriwa kuzingatia kuongeza wafanyakazi katika idara ya utalii kwani ni sekta muhimu kwa uchumi wa Lamu.

  • Tags

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Kiswahili ni ufunguo wa milango ya...

Kilimo: Wanafunzi 20 wa UoN wanufaika na mpango wa mafunzo...

T L