Habari Mseto

Serikali ya Lamu yaacha wanafunzi kwenye mataa

January 15th, 2019 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya wanafunzi 200 wa shule za sekondari kutoka jamii ya walio wachache ya Waboni, Kaunti ya Lamu wamelazimika kusalia vijijini na wazazi wao baada ya serikali ya kaunti ya Lamu ambayo ndiyo mfadhili mkuu wa wanafunzi hao kuchelewa kuwalipia karo mwaka huu.

Kulingana na jamii hiyo, wanafunzi kutoka eneo la Waboni wanadaiwa zaidi ya Sh 8 milioni za karo kwenye shule mbalimbali wanazosomea Lamu.

Katika mahojiano na wanahabari Jumatatu, wakazi wa jamii hiyo wakiongozwa na Mwakilishi wao wa Wadi, Barissa Deko, walieleza hofu kwamba huenda ndoto ya Waboni kusoma ikafifia iwapo serikali ya kaunti haitafanya jitihada ili kuwalipia wanafunzi hao karo.

Tangu jadi, jamii ya Waboni hutegemea msitu, ambapo huwinda wanyama pori, kuvuna asali ya mwitu na kuchuma matunda ya mwituni.

Aidha tangu serikali ya kitaifa kuzindua operesheni ya usalama ya Linda Boni kwenye msitu wa Boni mnamo 2015, dhamira kuu ikiwa ni kuwafurusha au kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha msituni humo, jamii ya Waboni imekuwa na ufukara kutokana na kufungwa kwa kitega uchumi chao.

Bw Deko aliilaumu serikali ya kaunti kwa kukosa kuwajibikia elimu ya Waboni.

Alisema licha ya kaunti kutenga mamilioni ya fedha kila mwaka ili kufadhili elimu ya wanafunzi kutoka jamii ya Waboni, inashangaza kwamba wanafunzi wao wamekuwa wakifukuzwa ovyo shuleni kwa ukosefu wa karo.

Bw Deko alisema wanafunzi wengi wa jamii yao wanadaiwa karo ya kati ya Sh 70,000 na Sh 80,000, hatua ambayo imewalazimu walimu wakuu wa shule husika kuwafurusha shuleni ili kutafuta karo ya kuendelezea masomo yao.

“Waboni ni jamii ndogo na ninashangaa kwamba licha ya mamilioni ya fedha kutolewa ili kukimu elimu ya wanafunzi wetu kila mwaka, wanafunzi hao hao wamekuwa wakifurushwa kila mara ili kutafuta karo. Ninaelezwa kwamba zaidi ya Sh 8 milioni zinadaiwa kama karo ya wanafunzi kutoka jamii yetu. Kaunti iwajibikie suala hilo ili wanafunzi wetu warudi kusoma. Waboni ni watu maskini na hawana namna ya kukimu karo ya watoto wao,” akasema Bw Deko.

Bw Yusuf Shalo, alieleza kutoridhishwa kwake na jinsi watoto wao wamekuwa kiguu na njia kila mara wakitafuta karo badala ya kubaki shuleni kusoma.

Alisema wanafunzi wao wanatoka vijiji vya mbali na kwamba kuna haja ya kaunti kuwajibika ili kuona kwamba watoto hao wanasalia shuleni kusoma.

“Kutoka Kiangwe hadi Lamu mjini ni zaidi ya kilomita 200. Hii inamaanisha punde watoto wetu wanapofukuzwa shuleni, sisi wazazi tunabeba jukumu la kuwasafirisha hadi vijijini mwetu, hali ambayo ni ghali mno kwetu. Kaunti itie bidii kuwalipia karo watoto wetu.

Bw Kuno Abdalla alisema huenda hatua ya kaunti kukosa kuwalipia karo Waboni ikawa ya makusudi ili jamii yao izidi kubakia nyuma kimaendeleo.

“Tayari tuko nyuma kimaendeleo na tunategemea elimu ya watoto wetu ili kuleta maendeleo eneo hili. Huenda kaunti haitaki kulipa karo kwa watoto wetu ili sisi Waboni tubaki nyuma kimaendeleo,” akasema Bw Abdalla.

Kwa upande wake aidha, Afisa Mkuu katika Idara ya Elimu ya Kaunti ya Lamu, Shee Sagara, alipinga madai ya kaunti kukosa kuwalipia karo wanafunzi wa jamii ya Waboni.

Badala yake, Bw Sagara alisema hivi majuzi kaunti ililipia Sh 15,000 za karo kwa kila mwanafunzi kutoka jamii hiyo.

Alisema huenda wale wanaolalamika kwamba kaunti haijawajibikia ulipaji wa karo si Waboni bali ni miongoni mwa watu wanaojidai kutoka jamii hiyo ili wanufaike.

“Tumelipia wanafunzi 165 kutoka jamii ya Waboni wanaosomea shule za sekondari za Hindi, Mokowe, Witu, Kiunga na Lamu Sh 15,000 kila mmoja hivi majuzi na mpango bado unaendelea. Wanolalamika kutolipiwa karo huenda ni watu ambao si wa jamii hiyo na ambao wanataka kunufaika na mpango huo,” akasema Bw Sagara.

Mbali na Waboni, afisa huyo alisema kaunti pia imetenga fedha za kutosha ili kufadhili karo kwa wanafunzi wote wa Lamu waliofanya mtihani wa KCPE na kujizolea alama 300 na zaidi.