Kimataifa

Serikali ya mpito: Majeshi na waandamanaji watofautiana

May 22nd, 2019 2 min read

Na AFP

UTATA kuhusu uongozi unazidi kukumba Sudan baada ya waandamanaji na wanajeshi jana kukosa kuafikiana kuhusu kuhusu muundo wa serikali ya mpito baada ya kung’olewa mamlakani kwa Omar al-Bashir mnamo Aprili 2019.

Wawakilishi wa pande zote walitofautiana vikali ikiwa serikali ya mpito itaongozwa na mwanajeshi au raia.

Mazungumzo kuhusu serikali ya mpito itakayojumuisha wanajeshi na raia yaling’oa nanga Jumapili lakini wakakosa kuafikiana.

Jumatatu, wawakilishi wa pande zote walikutana katika makao ya rais lakini mazungumzo hayo yakasambaratika baada ya kukosa muafaka.

Baraza la kijeshi lililochukua hatamu za uongozi baada ya kumng’oa Bashir, limekuwa likipata shinikizo kutoka kwa jamii za kimataifa inayotaka mamlaka yakabidhiwe raia.

Maelfu ya waandamanaji pia wamekataa kusitisha maandamano hadi pale jeshi litakapowakabidhi raia mamlaka.

Kiongozi wa waandamanaji Siddiq Yousef alisema kuwa mazungumzo hayo yameahirishwa hadi pale Baraza la Kijeshi linaloongoza nchi hiyo litakapokubali matakwa yao.

“Mvutano mkubwa uliopo ni kuhusu nani ataongoza serikali mpya ya mpito,” ikasema taarifa ya pamoja ya majenerali wa jeshi na viongozi wa waandamanaji.

Satea al-Haj, kiongozi wa vuguvugu linaloongoza maandamano, Alliance for Freedom and Change, alisema kuwa wanajeshi wanataka kiongozi wa serikali ya mpito awe mwanajeshi.

“Wanadai kuwa nchi inakabiliwa na tisho la ukosefu wa usalama hivyo wanahitaji kiongozi mwanajeshi kurejesha hali ya utulivu haraka iwezekanavyo,” akasema.

Serikali ya mpito

Waandamanaji wanasisitiza kuwa serikali ya mpito ni sharti iwe na idadi kubwa ya raia.

Wanataka kiongozi wa serikali ya mpito awe raia.

“Jamii ya kimataifa kama vile Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Kimataifa (UN) hawatakubali kushirikiana na serikali inayoongozwa na wanajeshi,” akasema Haj.

Licha ya utata huo, pande zote tayari wameafikiana mambo kadhaa. Wameafikiana kuwa serikali ya mpito iongoze kwa kipindi cha miaka mitatu na wabunge 300 watauliwe kutunga sheria.

Wamekubaliana kuwa idadi kubwa ya wabunge watateuliwa na mavuguvugu yanayoongoza maandamano.

Mazungumzo hayo yalisitishwa kwa zaidi ya saa 70 wiki iliyopita baada ya wanajeshi kususia wakitaka waandamanaji waondoe vizuizi walivyoweka katika barabara mbalimbali mjini Khartoum.