Habari

Serikali ya nusu mkate yaiva

June 28th, 2020 2 min read

Na SAMWEL OWINO

VYAMA vilivyotia saini mkataba wa ushirikiano na Chama cha Jubilee vimeanza kung’ang’ania usimamizi wa kamati kadhaa za Bunge ambapo nafasi ziliachwa wazi baada ya washirika wa Naibu Rais William Ruto waliokuwa wakizisimamia kutemwa.

Katika muda wa wiki chache zilizopita, Jubilee chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta imevutia vyama vya Wiper, Kanu, Chama Cha Mashinani, huku ODM kikiwa cha kwanza kwenye ushirikiano wake kutokana na handisheki ya 2018 kati ya Rais na kiongozi wa chama hicho Raila Odinga.

Imebainika kwamba, kando na nyadhifa za uongozi bungeni, vyama hivyo vinatarajia pia kunyakua nafasi katika Baraza la Mawaziri na usimamizi wa taasisi mbalimbali za serikali.

Hii ni kutokana na mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa katika baraza la mawaziri na uongozi serikalini kwa jumla wakati wowote sasa.

Katika Bunge la Kitaifa, chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka kinamezea mate uenyekiti wa kamati ya bajeti baada ya mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa kuondolewa, huku chama cha ODM kikitaka kuongoza kamati mbili.

Naibu Kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa, Robert Mbui aliambia Taifa Jumapili kwamba, Wiper imeomba Jubilee iruhusu mwanachama wake kusimamia kamati ya bunge kuhusu bajeti.

Bw Mbui ambaye ni mwandani wa Bw Musyoka alisema Wiper inataka mbunge wa Kitui ya Kati, Bw Makali Mulu kuongoza kamati hiyo.

“Iwapo tutaunga ajenda za Rais Kenyatta ambazo tulitia sahihi mkataba wa kufanya hivyo, basi ni lazima aonyeshe nia njema na kuruhusu tusimamie baadhi ya kamati,” akasema Bw Mbui.

Viongozi wa Jubilee wanataka mbunge wa Kieni, Kanini Kega kusimamia kamati hiyo muhimu.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema ni kiongozi wa chama atakayeamua watakaosimamia kamati za bunge.

“Maaumuzi hayo yatafanywa na kiongozi wa chama na iwapo nitapata, niko tayari,” alisema Kega.

Duru zingine zilisema Jubilee haitaki kuachilia uenyekiti wa kamati ya bajeti kwa sababu ya umuhimu wake wa kusimamia utayarishaji na utekelezaji wa bajeti ya kitaifa.

Kamati hiyo ina nguvu za kusimamia, kuchunguza na kushirikisha masuala yote kuhusu bajeti.

Rais Kenyatta hivi majuzi alisisitiza hatavumilia kufanya kazi na watu ambao hawana malengo sawa na yake.

Matamshi hayo yalichukuliwa kuashiria atatimua viongozi wote ambao wamekuwa wakimsaidia Dkt Ruto katika kampeni zake za mapema anapojiandaa kuwania urais 2022.

Chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, kinamezea mate uenyekiti wa kamati za Haki na Sheria na kile kiti cha Sheria za Ziada.

Hatua hiyo inamfanya Rais Kenyatta kujikuna kichwa kuhusu jinsi ya kumfurahisha mshirika wake wa kisiasa Raila Odinga.

Kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa, John Mbadi alisema hawajakubaliana kuhusu ugavi wa nyadhifa lakini mkutano umepangwa kufanyika wiki ijayo.

“Hatuna haraka, sasa tuko na siku 30 kujaza nafasi zilizoachwa wazi. Tulikubaliana na Bw Kimunya kwamba tutazungumza wiki ijayo,” alisema.

Wiki iliyopita, Bw Mbadi ambaye ni mwenyekiti wa ODM alisema kwamba chama kinataka kusimamia kamati ya Haki na sheria.

Kamati ya sheria ni muhimu hasa wakati huu ambao ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) inatarajiwa na mengi ya mapendekezo yake yatatekelezwa kupitia bunge na Rais Kenyatta na Bw Odinga hawataki kisiki wakati wa utekelezaji wake.

Mnamo Jumanne, bunge lilikubali kuongeza muda wa kujaza nafasi 16 kutoka siku saba hadi siku 30 ili pande zote zishauriane kuhusu wanachama wa kamati husika.

Bw Kimunya alisema angali mgeni katika wadhifa huo na kuunda upya kamati hizo kutahitaji muda kwa sababu kanuni za bunge hazikukusudia wabunge wengi wangeondolewa katika kamati mara moja.

Wiki jana, wabunge 16 wanaomuunga Dkt Ruto walivuliwa rasmi uanachama wa kamati tofauti katika zoezi linaloendelea la kuadhibu waasi katika chama cha Jubilee.

Wabunge wanne wandani wa Ruto walivuliwa uenyekiti wa kamati za bunge.

Wanne hao ni Julius Melly (Elimu) Ali Wario (Leba ) William Kisang (Habari na Mawasiliano) Joseph Limo (Fedha na Mipango) na Joash Nyamoko (Utangazaji).