Habari Mseto

Serikali ya Oparanya kujadili ripoti ya kufufua Mumias Sugar

August 15th, 2019 2 min read

NA BENSON AMADALA

RIPOTI ya Jopokazi lililoteuliwa na Gavana Wycliffe Oparanya kupendekeza mbinu ya kufufua kiwanda cha sukari cha Mumias tayari imewasilishwa kwa Baraza la Mawaziri la Kaunti ya Kakamega ili iweze kujadiliwa.

Waziri wa Biashara, Bw Kassim Were ambaye alikuwa mwenyekiti wa jopo hilo, jana alisema baraza la mawaziri litajadili namna mapendekezo ya kufufua kiwanda hicho yaliyomo kwenye ripoti hiyo yatakavyotekelezwa.

Bw Were alisema hayo huku wakulima wa miwa wakilalamika kuwa utawala wa Bw Oparanya ulikuwa ukijikokota kufichua mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo na mbinu ya kuitekeleza.

Kulingana na mapendekezo hayo, kiwanda cha Mumias kinafaa kushiriki kilimo cha miwa kwenye ekari 10,000 za ardhi ili kuzuia upungufu wa rasilimali hiyo ndipo iweze kuendeleza oparesheni zake bila tatizo lolote.

Hii ni kwa sababu hata viwanda vya miwa vinavyomilikiwa na watu binafsi vinaendelea kukabiliwa na uhaba wa miwa na mara nyingi hulazimika kuendesha shughuli zake na kukosa kutimiza malengo yake.

“Jambo hili ni kati ya masuala ambayo yataangaziwa kisha baraza la mawaziri liibuke na mbinu ya kuwasaidia wakulima wakati miwa inamea shambani kabla ya kukatwa na kuletwa kwenye kiwanda,” akasema Bw Were.

Waziri huyo aliongeza kwamba jopo hilo lilitekeleza wajibu wake kikamilifu baada ya kukutana na wakulima, wafanyakazi wa kiwanda cha Mumias, wenye hisa kwenye kiwanda hicho na mashirika yanayodai kiwanda hicho fedha.

“Baada ya baraza la mawaziri kujadili na kumkabidhi Bw Oparanya ripoti hiyo, atakuwa na mamlaka ya kuitoa kwa umma na kutekeleza mapendekezo yaliyomo ndani ya kufufua kiwanda cha Mumias,” akaongeza Bw Were.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Muungano wa Wakulima wa Miwa(KNFSF), Bw Ibrahim Juma jana alisema wakulima wameingiwa na hofu kutokana na kucheleweshwa kwa utekelezaji wa mapendekezo kwenye ripoti ya jopokazi hilo.

“Wakulima wa miwa wanasubiri kujua yaliyomo kwenye ripoti hiyo ili wafahamu iwapo mipango ya kufufua kiwanda cha Mumias bado ipo au la,” akasema Bw Juma.

Afisa huyo alisema wakulima watashawishika kuwekeza katika kilimo hicho wakielezwa hatua za kufanikisha kufufuliwa kwa kiwanda hicho.