Michezo

Serikali ya Taita Taveta kudhamini mbio za nyika za kaunti ndogo

January 16th, 2024 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

SERIKALI ya Kaunti ya Taita Taveta imeamua kwa mara ya kwanza kudhamini Mbio za Nyika za kaunti ndogo nne za Taveta, Wundanyi, Voi, na Mwatate ambazo zitafanyika Januari 20, 2023.

Waziri wa Michezo wa kaunti hiyo, Shadrack Mutungi amesema watagharimia utayarishaji wa viwanja vitakavyotumika, watalipia umeme na maji yatakayotumika kwenye viwanja hivyo, malipo ya maafisa wa huduma ya kwanza na watayarishi.

Bw Mutungi alisema mbali na hayo, pia watanunua maji na soda kuwapa wanariadha watakaoshiriki na maafisa watakaosimamia mbio hizo.

“Tumedhamini mbio hizi ili chipukizi wetu wapate fursa ya kuinua vipaji vyao vya riadha kufikia vya kimataifa,” akasema waziri huyo.

Mbali na udhamini wa mbio hizo za kaunti ndogo, Bw Mutungi alisema watadhamini na mashindano ya Mbio za Nyika na kaunti hiyo ya Taita Taveta yatakayofanyika katika uwanja wa Dawson Mwanyumba mjini Wundanyi hapo Januari 27, 2024.

“Wanariadha watakaochaguliwa pamoja na maafisa wa ufundi wa timu ya Taita Taveta itakayoshiriki Mbio za Nyika za Kanda ya Pwani mnamo Februari 10, 2024, tutagharamia kambi ya mazoezi kwa siku nne kabla ya kuelekea Kijiwetanga mjini Malindi kwa mbio hizo,” akasema.

Bw Mutungi aidha alisema watagharimia malazi na chakula kwa timu hiyo nyakati za kambi ya mazoezi na itakapokuwako Malindi na kuwapa nauli za kuenda makwao watakaporudi kutoka huko.

Mwenyekiti wa Chama cha Riadha cha Kenya (AK) tawi la Taita Taveta Dimmy Kisalu ameishukuru serikali ya kaunti hiyo kwa udhamini iliyoitoa kwani unawatia moyo wanariadha chipukizi.

“Haja yetu ni udhamini sio kupewa pesa. Kwa sababu serikali yetu itagharimia mbio zote na kuipeleka timu yetu huko Malindi, ni tosha kabisa. Tunaamini timu yetu itahifadhi mataji yao yote katika mbio za kanda,” akasema Kisalu.

Kisalu amefahamisha mbio za kaunti ndogo ya Taveta zitafanyika Sowene Primary na zile za kaunti ndogo ya Mwatate zitakuwa Kitivo Primary. Mbio za kaunti ndogo ya Wundanyi zitafanyika katika uwanja wa Dawson Mwanyumba na za kaunti ndogo ya Voi zitafanyika katika uwanja wa Moi.

Kaunti ya Taita Taveta imekuwa ikitawala mbio hizo za nyika kwa miaka mingi ambapo wakati huu inashikilia ubingwa na vikombe vyote vya mbio hizo.

Nahodha Panuel Mkungo ni mwanariadha anayeendelea kuwika ng’ambo mbio za Half Marathon na marathon.

Panuel Mkungo alipohifadhi taji lake la ubingwa wa Mbio za Nyika za Kaunti ya Taita Taveta za kilomita 10 kwa wanaume za mwaka 2023 katika uwanja wa Dawson Mwanyumba mjini Wundanyi mnamo Januari 7, 2023. PICHA | ABDULRAHMAN SHERIFF