Serikali ya Tanzania yakemea ulanguzi wa watoto walemavu

Serikali ya Tanzania yakemea ulanguzi wa watoto walemavu

NA WINNIE ONYANDO

SERIKALI ya Tanzania imeelezea masikitiko yake kuhusu filamu iliyopeperushwa na BBC ikionyesha jinsi walanguzi wa binadamu wanavyowalaghai wazazi walio na watoto walemavu na kuwaleta nchini kuwa ombaomba.

Alexander Lupilya wa sekretariati ya Kupambana na ulanguzi wa binadamu nchini Tanzania aliwashutumu wanaohusika katika biashara hiyo akisema wanakiuka haki za watoto hao walemavu.

“Tumesikitika sana kama serikali kuona filamu hiyo iliyopeperushwa na BBC ikionyesha namna watoto walemavu wanavyosafirishwa Kenya kuwa watumwa na kulazimishwa kuombaomba,” akasema Bw Lupilya.

Katika filamu hiyo, mwanahabari Njeri Mwangi anaonyesha jinsi wazazi wasiojiweza Tanzania hasa eneo la Mwanza wanavyolaghaiwa na kukubali kuwapa walanguzi watoto wao walemavu kuwa watumwa.

Baadhi ya wazazi hao wanaahidiwa maisha mazuri na kuambiwa watatumiwa pesa kila mwezi.Mwishowe, walanguzi hao wanawanyanyasa watoto hao kwa manufaa yao wenyewe.

Filamu hiyo iliyochukua zaidi ya mwaka mmoja kutayarishwa ilionyesha jinsi watoto walemavu wanaoishi katika mazingira magumu kutoka nchi jirani wanavyodanganywa na kuingia katika utumwa nchini.

“Wazazi wengi maskini nchini Tanzania wanakubali kuwapa walanguzi watoto wao baada ya kuhakikishiwa maisha mazuri. Lakini mwishowe, walanguzi hao huwatumia watoto kujinufaisha na kujipatia riziki,” akafichua Bi Njeri.

“Baada ya watoto kufika hapa Kenya, wanafanywa watumwa na kunyanyaswa. Kulazimishwa kuomba omba katika mitaa ya Nairobi kwa miaka mingi.”

Mwanahabari huyo siku moja alimfuata mlemavu mmoja aliyetambuliwa kama Bw Fara.

“Tulimfuata hadi Kariobangi ambapo tuligundua kwamba anazuiliwa na mlanguzi. Baadaye Bw Fara alifichua kwamba anadhulumiwa na kupigwa na mlanguzi wake ikiwa hajafikisha Sh2,000.”

Bw Fara amekuwa na mlanguzi wake aliyetambulika kama Zengo kwa muda wa miaka kumi.

Kulingana na utafiti huo, walanguzi hao wawili, Zengo na mwenzake wamekuwa wakiendeleza shughuli hiyo haramu nchini kwa miaka mingi.

Kila siku, walemavu hao husafirishwa kutoka ‘makazi’ yao Kariobangi na kusafirishwa kuombaomba katika maeneo mbalimbali Nairobi.

Siku moja, mwanahabari huyo pamoja na wenzake walimfuata Bw Fara hadi anakozuiliwa Kariobangi.

Waligundua kuwa si Bw Fara pekee anayezuiliwa katika jengo hilo bali kuna walemavu wengine pia wanaomtumikia Zengo.

“Baadaye, tuliwajulisha polisi kuhusu biashara hiyo inayoendeshwa kinyume na sheria.”

Polisi walimkamata Zengo na mwenzake na kuwaokoa walemavu wengine waliofungiwa kwenye chumba kimoja duni.

Washukiwa hao wawili walipinga tuhuma hizo na bado wanazuiliwa na polisi.

  • Tags

You can share this post!

Samboja awindwa tena kuhusu cheti cha chuo kikuu baada ya...

Divock Origi abanduka Liverpool na kuingia katika sajili...

T L