HabariSiasa

Serikali ya udikteta

June 6th, 2020 2 min read

Na MWANDISHI WETU

KENYA inaelekea katika utawala wa kidikteta iwapo hatua za Rais Uhuru Kenyatta kudhibiti vitengo huru vya serikali zitatumiwa kama kigezo.

Tayari ameweka ‘mfukoni’ Bunge la Taifa na Seneti, hali ambayo imewafanya wabunge na maseneta kupoteza uhuru wao na sasa ‘wanaimba tu wimbo’ wa Serikali Kuu.

Jaji Mkuu David Maraga pia amemuonya Rais Kenyatta dhidi ya kuingilia uhuru wa Idara ya Mahakama akitaja juhudi hizo kama ukiukaji wa Katiba.

Sawa na utawala wa chama kimoja, upinzani umezimwa kupitia handisheki ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, mbali na muungano wa Jubilee na vyama vingine vya kisiasa kuundwa.

Shutuma dhidi ya Rais Kenyatta kuhusu mienendo inayoonekana kuwa ya kiimla zilizidi kutokea wiki hii baada yake kutoa amri kuhusu mabadiliko ya utendakazi serikalini.

Mbali na amri ambayo ilimwondolea Naibu Rais William Ruto uhuru wa kusimamia afisi yake, ilibainika kuwa nakala hiyo kutoka kwa Afisi ya Rais ililenga kuvuruga uhuru wa Mahakama.

“Bunge limezimwa kikamilifu. Vyama vya kisiasa vimesalimu amri. Mahakama inaelekea kutekwa. Haya yote si ishara ya kumzima tu naibu mpotovu. Kuna nia nyingine kubwa,” aliyekuwa Seneta wa Mandera, Bw Billow Kerrow akaonya.

Kikatiba, asasi tatu kuu za utawala ambazo ni Bunge, Afisi ya Rais na Mahakama zimepewa uhuru wao kila mmoja.

Katiba inahitaji kuwa, uhuru wa Mahakama na asasi nyingine huru ikiwemo tume mbalimbali huru hazifai kuingiliwa kivyovyote na ushawishi kutoka nje.

Umuhimu wa uhuru huu ni kwamba, katiba ilinuia kuondoa mamlaka makubwa mikononi mwa rais kwani katika enzi zilizopita kabla katiba mpya kupitishwa mwaka wa 2010, marais walikuwa na mamlaka ya kutawala nchi jinsi walivyopenda bila kutoa nafasi ya kukosolewa na yeyote hata wakipotoka.

Wasiwasi kuhusu kutekwa kwa vitengo huru vya kitaifa unatokea wakati ambapo Rais amebakisha muda mfupi kabla ahitajike kustaafu kikatiba katika mwaka wa 2022.

Wadadisi wa masuala ya uongozi wanasema kuwa, ni kawaida kila wakati Uchaguzi Mkuu unapokaribia viongozi wa mataifa kufanya marekebisho kwa uongozi wao.

Hata hivyo, imeonekana kuwa wale wanaopuuza sheria na katiba za nchi zao wanapofanya mabadiliko hayo, huwa wana kusudi la kukwamilia mamlakani kinyume na sheria.

“Huu ni wakati kwa kila mwanasiasa, mashirika ya kijamii, na viongozi wa kidini kuungana ili kukomesha taifa kurudishwa kwa utawala wa kiimla. Lazima tukomeshe mwelekeo huu wa Uhuru Kenyatta sasa la sivyo tutaishi kujuta,” akasema mtaalamu wa masuala ya uongozi, Dkt David Ndii.

Jaji Mkuu David Maraga alikosoa sehemu ya amri ya Rais ambayo ilifanya mabadiliko kwa majukumu ya mahakama.

Katika amri hiyo, Rais Kenyatta alikuwa amesema ametumia mamlaka yake ya kikatiba ya kuagiza na kusimamia majukumu ya wizara na idara za serikali.

“Mahakama si wizara wala idara ya mahakama ambayo inaweza kusimamiwa na amri ya rais. Vivyo hivyo, amri ya rais haiwezi kugeuza wala kugawa kazi kwa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) wala Mwenyekiti wake,” akasema Jaji Maraga.

Alisisitiza kwamba JSC na Mahakama kwa jumla ni asasi huru zisizofuata maagizo ya Afisi ya Rais, na hili linafaa kutambuliwa na kuekwa wazi katika maagizo yoyote yanayotolewa na Serikali Kuu.

“Ningependa kuamini kwamba agizo hilo lilitolewa kimakosa na kwamba Afisi ya Rais itafanya marekebisho,” akasema.

Kinyume na maagizo mengine ambayo yamewahi kutolewa na Afisi ya Rais, agizo hilo la majuzi lilitolewa kisiri bila nakala yake kutumwa kwa vyombo vya habari jinsi ilivyo desturi.