Habari Mseto

Serikali yaagizwa kuwalipa wanakandarasi wote

November 22nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Wizara na taasisi zote za serikali zimeagizwa kuwalipa watoaji wa huduma, bidhaa na wanakandarasi kabla ya kutuma maombi mapya.

Kufikia sasa, madeni ya serikali ya kitaifa kwao ni Sh29.3 billion katika mwaka wa kifedha wa 2017/18 kulingana na ripoti ya Wizara ya Fedha.

“Serikali imelipa suala la kulipa madeni yaliyotokana na kupewa huduma na bidhaa kipau mbele. Hivyo, wizara, idara na taasisi za serikali zinaagizwa kulipa madeni katika mwaka wa kifedha wa 2018/2019,” ilisema ripoti hiyo.

Wizara, idara na taasisi za serikali katika muda wa miezi mitatu kufikia Septemba 2018 zilitumia Sh437.6 bilioni dhidi ya Sh262.4 bilioni zilizolengwa.

Fedha nyingi zaidi zilitumiwa kulipa mishahara, pensheni na riba (Sh194.3 bilioni) dhidi ya Sh268.2 bilioni zilizotarajiwa ilhali wizara na mashirika hayo yalitumia Sh68.1 bilioni za maendeleo dhidi ya Sh169.3 bilioni zilizolengwa.

Kulingana na Wizara ya Fedha, wizara, idara na mashirika ya serikali hayakuripoti pesa zote zilizotumika.