Habari Mseto

Serikali yaagizwa iwafidie Sh51 milioni watu iliyowafurusha nchini

March 14th, 2018 1 min read

Jaji George Odunga akiwa katika mahakama kuu alipoamuru watu 12 walipwe fidia ya zaidi ya Sh51milioni na Serikali. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

SERIKALI  Jumanne iliamriwa iwalipe watu 12  walikamatwa na kupelekwa  nchini Somalia miaka 11 iliyopita fidia ya zaidi ya Sh51 milioni.

Kumi na wawili hao walitiwa nguvuni wakati wa msako na badala ya kushtakiwa kortini walipelekwa moja kwa moja hadi Somalia.

Kati yao, walalamishi wawili walikuwa raia wa Tanzania na mmoja raia wa Rwanda.

Baadaye walihamishwa kutoka Somalia wakapelekwa nchini Ethiopia.

Mahakama iliambiwa walalamishi hao waliteswa kwa vile hakuna ushahidi uliowasilishwa kuthibitishwa walikuwa humu nchini wakitekeleza uhalifu.

Walalamishi hawa Mabw Salim Awadh Salim, Saidi Hamisi Mohamed, Bashir Hussein Chirag, Mohamed Sader, Hassan Shabani Mwazume, Swaleh Ali Tunza, Abdallah Halfan Tondwe, Kasim Musa Mwarusi na Ali Musa Mwarusi (Wakenya) nao Fatma Ahmed Chande na Mohamed Abushir Salim (raia wa Tanzania) na Clement Ibrahim Muhibitabo, raia wa Rwanda waliondolewa nchini Kenya kwa vile walikuwa Waislamu.

Jaji George Odunga aliiamuru Serikali iwalipe fidia ya Sh51,261,031 na  faida tangu 2014 wakati uamuzi uliposomwa na Jaji Mumbi Ngugi aliyesikiza kesi hiyo kwamba washtakiwa walitiwa nguvuni kinyume cha sheria.

Mnamo Jumanne walalamishi walimsihi  Jaji Odunga aamuru serikali iwalipe kama ilivyoagizwa la sivyo katibu wa usalama asukumwe ndani kwa kukaidi agizo la korti.