Habari Mseto

Serikali yaambia wazazi walipe karo hata kama shule zimefungwa

May 29th, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

WAZIRI wa Elimu Profesa George Magoha ametaka wazazi ambao watoto wao wanasoma katika shule za wamiliki binafsi waendelee kulipa karo.

Akitangaza kuwa shule hazitafunguliwa wakati wowote hivi karibuni kwa sababu ya janga la corona, Prof Magoha alitaka wazazi wajadiliane na wasimamizi wa shule za wamiliki binafsi kuhusu watakavyolipa karo ya muhula wa pili.

Ijumaa, serikali ilitangaza maambukizi mengine 127 ya virusi vya corona na kupelekea idadi ya jumla ifike 1,745.

Nao watu wanne walifariki Mombasa na kufikisha idadi ya waliokufa hadi 62, na 17 wakapona na kuongeza idadi ya waliopona hadi 438.

Wazazi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa shule zimekuwa zikiwataka walipe karo ya muhula wa pili ilhali watoto wako nyumbani kufuatia agizo la serikali la kuzifunga ili kuzuia maambukizi ya corona.

Baadhi ya shule za kibinafsi zimekuwa zikitoa mafunzo kupitia mitandao na zinataka mafunzo hayo yalipiwe.

Waziri Magoha alisema shule hizo hutegemea karo kulipa mishahara ya walimu na wafanyakazi wapatao zaidi ya 300,000 kitaifa.

“Ninachoweza kuwaambia wazazi ni kuwa waende kujadiliana suala la karo na wasimamizi wa shule. Kuna walimu na wafanyakazi wanaohitaji mishahara ili wajikimu kimaisha na shule hizi hutegemea karo hiyo,” alisema.

Prof Magoha alisema wazazi wakikosa kulipa karo, shule za wamiliki binafsi zitaporomoka na wanafunzi wote kuhamishiwa shule za umma.

“Ili kulinda shule hizo, itakuwa makosa kusema wazazi wasilipe karo. Walipopeleka watoto katika shule hizo walijua lazima karo ilipwe,” alisema.

Alikuwa akizungumza baada ya kupokea ripoti kutoka kwa jopo ambalo lilipokea maoni ya wananchi kuhusu kama shule zinastahili kufunguliwa.

Alisema imeamuliwa shule zitafunguliwa tu wakati ambapo usalama wa wanafunzi na walimu utahakikishwa.

Waziri huyo alisema kuwa kwa sasa hali ya maambukizi ya corona hairuhusu shule kufunguliwa.

Mnamo Jumatano, vyama vya walimu na wahadhiri vilisema shule hazifai kufunguliwa kabla ya Septemba 2020.