Habari Mseto

Serikali yaanza kulipa fidia wenye mashamba ya SGR

December 18th, 2018 1 min read

Na ERIC MATARA

WATU zaidi ya elfu moja walioathiriwa na awamu ya pili ya ujenzi wa reli mpya ya kisasa (SGR) kati ya Nairobi na Naivasha wanaendelea kufidiwa mashamba na mali yao.

Kaimu Mwenyekiti wa Tume ya Ardhi (NLC), Bi Abigael Mukolwe alisema wanaofidiwa ni watu 1,810 ambao wanaishi au wako na mali kati ya mbuga ya wanyama ya Nairobi hadi kituo cha reli cha Rongai, Kaunti ya Nakuru.

Bi Mukolwe alisema tume imepokea Sh7.2 bilioni itakazotumia kufidia watu hao.

Alisema serikali imekamilisha kuandaa fidia ya mali iliyo eneo ambayo reli hiyo itapitia kati ya Naivasha na Suswa Kaunti ya Narok.

Pesa hizo zitakuwa afueni kwa wenye ardhi ambao awali walilemaza ujenzi wa reli hiyo wakilalamikia kucheleweshwa kwa fidia ya mashamba yao.

“Shughuli ya ulipaji fidia inaendelea vyema. Tunasubiri pesa zaidi kutoka kwa Shirika la Reli kuwafidia wamiliki wa ardhi walioathiriwa na awamu ya pili ya ujenzi wa SGR,” alisema Bi Mukolwe. Alisema wamekuwa wakilipa fidia baada ya kukagua hati miliki za wanaonufaika.

Wakati huo huo, Bi Mukolwe aliwaambia watakaonufaika kutumia vizuri pesa watakazolipwa.

“Tumekuwa tukiona baadhi ya wanaofidiwa mashamba yao wakitumia vibaya pesa zao na kubaki masikini. Ninawashauri watakaonufaika kuhakikisha kwanza wamepata makao mapya na kuepuka ushawishi unaojiri na kuwa mamilionea mara moja ,” aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano.

Fidia ya mashamba hubadilika kuwa laana kwa wanaonufaika huku wakitumia vibaya pesa hizo. Kwa mfano, waliolipwa fidia wakati wa ujenzi wa awamu ya kwanza ya SGR kati ya Mombasa na Nairobi walitumia vibaya pesa hizo na sasa wamebaki masikini.