Habari

Serikali yaanza kupanda miche ya miti katika msitu wa Mau

November 1st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imezindua mpango wa upanzi wa miche ya miti katika msitu wa Maasai Mau,  Kaunti ya Narok, kama sehemu ya mchakato wa kuutunza.

Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko ameongoza shughuli hiyo kuanzia Ijumaa asubuhi ambapo amepanda mti eneo la Sierra Leon, Maasai Mau katika mpango wa uhifadhi wa mazingira kwa kusudi la kuvilinda vyanzo vya maji.

Amesema serikali ina nia njema ya kuhakikisha raia wake wanaishi katika mazingira salama.

“Wakati wa ufurushaji wa waliokuwa wanaishi hapa msituni kinyume cha sheria, maafisa na vyombo vya usalama havikujali huyu ni wa jamii gani na yule ni wa jamii gani,” amesema waziri Tobiko.

Ameongeza kwamba wote waliokuwa humo ama wawe ni wa jamii za Maasai, Kisii au jamii nyingine ile, walilazimika kuondoka na wala sio kwamba jamii fulani ilikuwa inalengwa.

Mwishoni mwa Oktoba 2019, kamishna wa kanda ya Rift Valley George Natembeya kwenye taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari alisema mawaziri kadhaa, wakiongozwa na waziri wa Mazingira na Mali Asili Keriako Tobiko, wangehudhuria shughuli hiyo ya leo Ijumaa, Novemba 1.

“Baada ya kukamilika kwa matakaa ya watu waliokuwa wakiishi katika msitu wa Maasai Mau kinyume cha sheria kukamilika Jumamosi, wiki ijayo )(leo Ijumaa) serikali itaanza kurejesha msitu huu katika hali yake ya zamani kwa kupanda miti. Kwa ujumbe tunapanga kupanda miche milioni 13 katika shughuli ambayo itaongozwa na Waziri Keriako Tobiko na wenzake,” akasema Bw Natembeya.

Bw Natembeya alisema idadi kubwa ya waliokuwa wakiishi katika msitu huo kinyume cha sheria wameondoka na wanaosalia wataondolewa kwa njia ya kiutu.

Msitu wa Maasai Mau wenye ukubwa wa hekta 46,000 ni sehemu ya msitu mpana wa Mau ambao umesambaa katika kaunti angalau tano.

Kaunti hizo ni pamoja na Nakuru, Kericho, Narok, Bomet na Uasin Gishu.

Msitu huo ni mojawapo ya chemchemi tano kubwa ya maji nchini na ni chanzo cha mito inayoelekeza maji katika mbuga ya Maasai Mara na eneo la Serengeti.

Duru zinasema kuwa zaidi ya familia 500 zilizohama kutoka Maasai Mau wakati huu zimepiga kambi karibu na Kanisa la AIC Torokwo, eneo la Olenguruone huku zikitafakari namna ya kujisaidia.

Wengi wao wanalalamika kuwa waliuza mashamba ya manyumbani mwao kisha wakanunua ardhi katika Msitu wa Mau na ndio maan hawana pa kuenda.