Habari Mseto

Serikali 'yachapisha' pesa mpya kufufua uchumi

October 6th, 2020 1 min read

NA FAUSTINE NGILA

SERIKALI ‘imechapisha’ fedha mpya za Sh15 bilioni katika kipindi cha siku saba kufikia Septemba 25, kulingana na takwimu kutoka Benki Kuu ya Kenya (CBK).

Serikali ilipokea Sh46 bilioni kama mkopo wa muda kutoka CBK ambazo ni ongezeko kutoka Sh31.3 bilioni wiki iliyotangulia.

Fedha hizo ndizo mkopo wa juu zaidi ambao serikali imechukua kutoka CBK kwa wiki moja, na ulijiri katika kipindi ambapo Hazina Kuu inashinikizwa kulipa riba.

Katika mpango wa aina hiyo, CBK kwa kawaida hutuma fedha kwa akaunti za serikali, mchakato ambao unaitwa ‘kuchapisha pesa’.

Lakini ikiwa pesa nyingi zimechapishwa, wananchi wanaweza kudai bidhaa nyingi sokoni, na iwapo kampuni zinaendelea kuwa na kiasi sawa cha bidhaa, basi zitalazimika kupandisha bei.

Hazina Kuu imekabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha kutokana na athari za virusi vya corona, na kulazimika kuomba pesa nyingi kutoka kwa soko la humu nchini kujairbu kuokoa uchumi.

Kufikia mwishoni mwa mwaka wa kifedha wa 2019/2020, serikali ilikuwa imeomba Sh47 bilioni.