Michezo

Serikali yafunga mlango wa nyuma ambao SportPesa ilinuia kutumia kerejea kwa biashara

October 31st, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO MLANGO wa nyuma ambao kampuni ya kubashiri matokeo ya michezo SportPesa ilinuia kutumia kurejea kwenye biashara umefungwa Jumamosi na serikali.  Bodi ya Kudhibiti Kamari na Utoaji wa Leseni nchini (BCLB)  imesitisha mara moja kampuni ya Milestone Games Limited kuendesha shughuli zake humu nchini chini ya jina la SportPesa. Kwa mujibu wa BCLB, SportPesa ni jina la kibiashara linalohusishwa rasmi na Pevans East Africa na hivyo, hatua ya kutumiwa na mmiliki wa kampuni nyingine ni ukiukaji wa sheria. Maamuzi ya kurejea kwa SportPesa katika soko la mchezo wa kamari nchini Kenya yalifichuka mnamo Oktoba 30, siku ambayo Afisa Mkuu Mtendaji wa SportPesa Ronald Karauri alitangaza marejeo ya jina hilo la kibiashara chini ya kampuni mpya inayomiliki leseni ya BCLB. “Kwa mujibu wa taarifa tuliyonayo, jina ‘SportPesa’ ni la M/s Pevans East Africa Limited. Kampuni hiyo imekata rufaa katika Mahakama ya Rufaa jijini Nairobi kesi nambari 471 ya 2019. Kesi hiyo inalalamikia msingi wa kutolewa kwa leseni ya Pevans East Africa kwa mmiliki tofauti na itasikizwa Novemba 16, 2020,” akasema Mwenyekiti wa BCLB, Cyrus Maina katika barua yake kwa Meneja wa Milestone, Bernard Chauro.
“Hivyo, unazuiwa kutumia jina la kibiashara la ‘SportPesa’, wavuti wa www.ke.sportpesa.com, www.sportpesa.co.ke, kodi fupi za 29050 na 79079 na nambari za malipo kwa njia ya simu za Pay Bill 521521, 9555700 na 955700 hadi pale ambapo Mahakama ya Rufaa itafanya maamuzi ya kesi iliyoko kortini na mpaka wakati ambapo Bodi itashughulikia ombi lako la kutwaa umiliki wa vyote vilivyotajwa hapo juu,” ikaendelea taarifa.
BCLB hata hivyo ilikariri kwamba Milestone wako huru kuendelea kutumia jina la kibiashara la ‘Milestone Bet’ kupitia wavuti www.milestonebet.co.ke, www.milestonegames.co.ke, na www.milestonegames.com. Bw Maina alishikilia kwamba maamuzi ya kunyima Milestone idhini ya kutumia jina ‘SportPesa’ pamoja na miundo-misingi nyingine ya kiteknolojia inayohusishwa na Pevans East Africa ni ya kimakusudi ili kuzuia tukio la kukanganya umma. “Sababu kuu ni kwamba kuna tofauti kubwa katika jina linalopendekezwa na Milestone Games Limited kwa minajili ya matumizi yao na idhini ya kulitumia jina ‘SportPesa’ italeta mkanganyiko zaidi miongoni mwa wananachi,” akasema. SportPesa ni jina maarufu zaidi miongoni mwa washiriki wa michezo ya kamari hasa katika ulingo wa soka ya humu nchini na leseni ya kampuni hiyo ilitwaliwa na Serikali mnamo Oktoba 2019 baada ya kampuni hiyo kuhusishwa na tukio la kukosa kulipa ushuru wa hadi Sh15.1 bilioni.
Hatua ya Milestone ya kutumia jina ‘SportPesa’ imefasiriwa kuwa hatua ya kimakusidi ya kutaka kuchuma nafuu kutokana na zaidi ya wateja milioni 12 kwenye data kanzi ya SportPesa, na ambao walikuwa wakishiriki mchezo wa kamari kupitia kampuni hiyo ya Pevans East Africa Limited.
Kwa mujibu wa BCLB, Milestone walikuwa wameidhinishwa kutumia jina SportPesa kwa miaka mitano na kampuni ya Sportpesa Global Holdings ambayo ina wakurugenzi sawa na wale wanaohudumu katika kampuni ya Pevans East Africa. Panda-shuka zinazoshuhudiwa katika vita vya uhalali na uharamu wa kutumiwa kwa jina la SportPesa ni ishara za ukubwa wa kiwango cha kutofuatiana kwa waanzishilishi na wadhamini wa jukwaa la michezo ya kamari la SportPesa na Pevans East Africa kwa ujumla.