Serikali yafuta kandarasi ya kiwanda cha samaki

Serikali yafuta kandarasi ya kiwanda cha samaki

IBRAHIM ORUKO

SERIKALI imesitisha kandarasi ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha samaki cha Liwatoni Kaunti ya Mombasa, ambacho ni mojawapo ya miradi muhimu ya Rais Uhuru Kenyatta eneo la Pwani.

Kiwanda hicho ambacho Rais Kenyatta ametambua kama mradi muhimu wa kuimarisha uchumi wa baharini, kilinuiwa kubadilisha Liwatoni kuwa bandari kamili ya uvuvi ikiwa na vyumba vya barafu vya kuhifadhi samaki na ambapo serikali itaongezea thamani samaki kabla ya kuuzwa nje ya nchi.

Kufutwa kwa kandarasi hiyo kutahujumu mipango ya Rais Kenyatta na nafasi ya kuimarisha uvuvi kwenye bahari.

Kampuni ya Daniel’s Outlets Ltd ilipatiwa tenda ya kujenga kiwanda hicho lakini serikali imeilaumu kwa kukiuka masharti ya ujenzi hatua iliyoifanya kusitisha kandarasi.

Katibu wa idara ya uvuvi na uchumi wa baharini Dkt Francis Owino, alilaumu mwanakandarasi kwa kuhusika na ufisadi na ulaghai na kuagiza kampuni hiyo kuondoka eneo la ujenzi mara moja.

Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), pia imeanza kuchunguza madai ya hitilafu katika utoaji wa tenda hiyo.

Katika uamuzi wake wa kusitisha kandarasi hiyo, katibu alitaja uchunguzi unaofanywa na EACC na baadhi ya masharti ya kandarasi.

Kipengee cha 15.2 (f) ambacho katibu alitaja kinapatia serikali nguvu za kusitisha kandarasi iwapo mwanakandarasi atatoa au kuahidi kutoa hongo, zawadi au kiinua mgongo kwa mtu yeyote, moja kwa moja au kupitia mtu mwingine ili apatiwe tenda.

Mnamo Aprili 1 2021, Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Twalib Mbarak alimwandikia barua Dkt Owino kumfahamisha kuhusu uchunguzi ambao tume inafanya na kumuomba asimamishe malipo kwa mwanakandarasi hadi uchunguzi ukamilike.

“Kwa kutekeleza majukumu yake ya kikatiba na kisheria, EACC imeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya hitilafu katika utoaji wa zabuni ya kandarasi,” Bw Mbarak alisema kwenye barua yake kwa katibu ambayo alinakili kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ambaye ni mwenyekiti wa kamati tekelezi ya miradi ya maendeleo ya serikali ya kitaifa.

“Tunakushauri kwamba malipo yoyote yanayohusiana na kandarasi hii yanafaa kusimamishwa hadi uchunguzi utakapokamilika,” ilisema barua ya Bw Mbarak.

You can share this post!

Gavana bado katika hatari

Jinsi janga la Covid-19 lilivyochangia kuongezeka kwa visa...