Serikali yaibuka na mikakati ya kushusha gharama ya chakula cha mifugo

Serikali yaibuka na mikakati ya kushusha gharama ya chakula cha mifugo

NA SAMMY WAWERU

JUMA lililopita, Waziri wa Kilimo Peter Munya alitangaza kusitisha kwa muda ada na ushuru unaotozwa mahindi na malighafi yanayotumika kutengeneza chakula cha mifugo, yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa maelezo ya waziri inalenga kushusha bei ya unga wa mahindi na chakula cha mifugo kwa muda wa siku 90 zijazo, kabla msimu wa mavuno kuanza.

Chini ya kipindi cha muda wa miaka miwili iliyopita, bei ya malisho ya mifugo imekuwa ikiongeza kila uchao.

Unga wa mahindi nao unazidi kuwa ghali, wakati ambapo wananchi wanaendelea kulemewa na gharama ya juu ya maisha na uchumi.

“Hatua tulizochukua zitasaidia kuleta nafuu, tukishughulikia kukwamua matrela ya mahindi mpakani ambapo msongamano unashuhudiwa,” waziri akasema.

Kulingana na Katibu katika Idara ya Ufugaji Harry Kimtai serikali imeibuka na mikakati kusuluhisha kero ya kupanda kwa chakula cha mifugo nchini.

Katibu katika Idara ya Ufugaji Bw Harry Kimtai. PICHA | SAMMY WAWERU

Kando na mpango wa muda kuondoa ada na ushuru, Bw Kimtai anasema serikali inatathmini marufuku ya nafaka zilizoboreshwa (GMO).

“Tunaendelea kutathmini sheria za mahindi ya GMO, yanayoagizwa kutoka nje ya nchi na malighafi mengineyo ya nafaka zilizoboreshwa ambazo hutumika kuunda chakula cha mifugo,” Katibu asema, akisisitiza i makini kuhusu suala hilo.

Kenya huagiza kutoka nje karibu asilimia 80 ya malighafi kuunda malisho ya mifugo.

Mahindi, shayiri (barley), soya, ngano, alizeti (sunflower) na mbegu za pamba ndiyo malighafi yanayotumika kuyatengeneza.

Serikali iliidhinisha ukuzaji wa pamba iliyoimarishwa – BT Cotton, mahindi yakiendelea kufanyiwa utafiti na uchunguzi.

Zao lingine lililoidhinishwa, japo linafanyiwa majaribio ni mihogo.

Utafiti huo unashirikisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Kalro), watafiti na Wanasayansi.

Wadudu aina ya BSF

Bw Kimtai ameiambia Taifa Leo kwamba, mpango mwingine kusaidia kushusha gharama ya chakula cha mifugo ni kupitia ufugaji wa wadudu aina ya BSF – Black Soldier Flies.

“Ni muhimu kuwa na njia mbadala, na tunahimiza vijana wajitokeze na kujituma kufuga BSF,” aelezea.

Wadudu hao wanasifiwa kuwa na kiwango cha juu cha Protini, na ni bora katika utengenezaji wa chakula cha mifugo.

“Mpango wa kudumu, ni kutumia ardhi za serikali zisizotumika kutoka idara zote, hususan maeneo yenye hali bora ya hewa kuendeleza kilimo cha nyasi na nafaka,” Kimtai adokeza.

Kulingana na afisa huyu, mkakati huo utajumuisha wawekezaji wa kibinafsi kukuza nafaka na nyasi za mifugo.

“Kwa sasa, tunakusanya data za idadi ya mashamba yatakayotumika na kuibuka na mpangilio maalum kukodisha wawekezaji ili kuepuka unyakuzi wa ardhi,” afafanua.

Kaunti ya Kajiado, baadhi ya wawekezaji wa kibinafsi wametoa mfano mzuri kuzindua maeneo na vituo vya kulishia mifugo (feed lots).

Vituo hivyo aidha vinasifiwa kusaidia kuokoa mifugo kero ya kiangazi na ukame inapokithiri.

  • Tags

You can share this post!

Muruli aahidi uwazi baada ya kuchaguliwa kuongoza tawi la...

Kocha Duncan Ferguson aagana na Everton ili ajikuze zaidi...

T L