Habari Mseto

Serikali yaimarisha ukaguzi wa Ebola mpakani

July 2nd, 2019 1 min read

Na GERALD BWISA

SERIKALI imeimarisha uchunguzi mpakani kati ya Kenya na Uganda, ambapo imetoa mafunzo kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kwa wahudumu wa afya 310 na wanajamii wa kujitolea 400.

Afisa Mkuu Msimamizi wa Afya Kaunti ya Trans Nzoia Bi Clare Wamalwa alieleza kuwa maeneo saba yametengwa na vile vile uchunguzi kwa saa 24 kuanzishwa eneo la mpakani la Suam.

Akiongea wakati wa mkutano miongoni mwa washikadau katika sekta ya afya, Bi Wamalwa alisema kundi la kukabiliana na Ebola limebuniwa ili kuimarisha kampeni dhidi ya ugonjwa huo hatari.

“Wahudumu 310 na wanajamii 400 wa kujitolea wamepewa mafunzo kuhusiana na jinsi ya kutambua na kuzuia maambukizi ya Ebola. Tumeanzisha vituo saba vya kutibu Ebola katika kaunti ya Trans Nzoia,” alisema.

Vituo vitatu vimeanzishwa eneo la Endebess karibu na mpaka wa Kenya na Uganda, vituo viwili eneo la Kwanza na vingine viwili katika Hospitali ya Rufaa ya Kitale.

Alisema serikali ya kitaifa inashirikiana na serikali za kaunti kuimarisha uchunguzi eneo hilo ambalo linakabiliwa na hatari ya maambukizi ya ugonjwa huo kwa sababu ya mpaka wazi.

Afisa huyo wa afya alisema kampeni ya kuhamasisha umma imeanzishwa na vifaa vya matibabu kutolewa.

“Zaidi ya kununua vifaa muhimu, tumehusisha mashirika mengine kuhamasisha umma,” alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na wananchi wengi wanaozuru Kenya au Uganda, shughuli za uchunguzi wa maambukizi ya Ebola zimeimarishwa, na kuongeza kuwa wafanyabiashara wamehamasishwa kuhusu ugonjwa huo.

Mkurugenzi wa Afya Dkt Gilbert Suwon alisema mpaka wazi umeibua changamoto kubwa katika utekelezaji wa kampeni dhidi ya maambukizi ya Ebola.