Habari za Kitaifa

Serikali yaingia baridi, yaondoa Mswada kubadilisha Sheria za Ardhi

Na DAVID MWERE July 1st, 2024 1 min read

HOFU ya kuibua hasira za umma kwa kujaribu kurekebisha katiba kupitia mlango wa nyuma ililazimisha serikali kuondoa Mswada wenye utata wa Sheria za Ardhi (Marekebisho) wa 2023 ambao tayari ulikuwa unajadiliwa katika Bunge la Kitaifa.

Wakati wa kuuondoa mswada huo ambao ulilenga kuanzisha ushuru wa kila mwaka wa ardhi kwa kupunguza mamlaka ya kikatiba ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kwa kuhamisha majukumu yake makuu kwa Wizara ya Ardhi, ulikuwa mbele ya kamati ya Ardhi ya Baraza la Mawaziri.

Mswada huo, uliowasilishwa na kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah, ulitaka kufanyia marekebisho Sheria sita za Ardhi- Sheria ya Usajili wa Hatimiliki, Sheria ya Udhibiti wa Ardhi, Sheria ya Usajili wa Ardhi, Sheria ya Ardhi, Sheria ya Ardhi ya Jamii na Sheria ya Mali.

Akiwa kiongozi wa wengi na mbunge wa Kikuyu, Bw Ichung’wah, anatia saini Miswada yote ya serikali iliyowasilishwa katika Bunge la Kitaifa.

Akifahamu upinzani kwa Mswada huo kutoka kwa umma, mnamo Juni 13, 2024, Bw Ichung’wah alieleza rasmi nia ya serikali kwa kumwandikia Spika wa Bunge Moses Wetang’ula nia yake ya kutaka Mswada huo uondolewe.

“Baada ya kushauriana na washikadau husika, na thibitisha kwamba chama cha walio wengi kimeondoa Mswada huo,” akasema Bw Ichung’wah katika barua kwa Spika.

Kutokana na hali hiyo, Bw Ichung’wah aliitaka Kamati ya Shughuli za Biashara ambayo inaongozwa na Spika na ina wajibu wa kuweka vipaumbele shughuli zinazopaswa kushughulikiwa na Wabunge, ijulishwe kuhusu kuondolewa kwa Mswada huo.

NLC ilipewa mamlaka ya kuongoza mageuzi ya ardhi nchini.

Licha ya hayo, Mswada ulitaka kuhamisha majukumu mawili makuu ya NLC- uthamini wa ardhi na utwaaji wa ardhi kwa niaba ya Serikali ya Kitaifa na Serikali za Kaunti hadi kwa Wizara ya Ardhi.