Habari za Kitaifa

Serikali yajigamba ikisema ETA imeongeza wageni na mihela

January 12th, 2024 1 min read

NA NDUBI MOTURI

SERIKALI imejigamba ikisema mfumo wa kielekroniki wa kutoa vibali vya kufanikisha usafiri kwa wanaoingia nchini (ETA) ni madhubuti na umeimarisha nafasi ya Kenya kimataifa kama kivutio cha wengi.

Kufikia sasa maombi ya 25,000 ya ETA yamefanikishwa, Kenya ikivuna Sh159 milioni kutoka kwa raia wa kigeni wanaoingia nchini au kupitia nchini wakielekea kwa mataifa mengine.

Katibu wa Uhamiaji na Huduma kwa raia, Prof Julius Bitok hata hivyo alisema Alhamisi kwamba maombi 110 kwenye mfumo huo yalikataliwa kwa sababu za kiusalama.

Maombi 7,000 yangali yanashughulikiwa.

Prof Bitok alisema kwamba, mfumo wa ETA ambao ulianza kazi wiki moja iliyopita, umeimarisha safari za wanaotaka kuzuru Kenya maradufu.

“Mfumo wa ETA ndiyo mambo yote katika dunia ya kisasa kwani umepunguza muda wa wageni kupata vibali kuingia nchini. Vile vile idadi ya watalii imeongezeka maradufu,” akasema Prof Bitok.

Katibu huyo alisema inamchukua mtu dakika tano pekee kutuma ombi, nao maafisa huidhinisha kulingana na tarehe ambayo mgeni anataka kuingia nchini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Uhamiaji Evelyn Cheluget alisema serikali inapokea maoni na kufanya maboresho kwa mfumo huo.

“Tayari tumeondoa hitaji la taarifa za kutoka benki kwenye mfumo huo na kupunguza muda hadi dakika tano,” akasema Bi Cheluget.

Ada kwa kila anayetuma ombi ni Dola 30 au (Sh4,762.50).

Rais William Ruto mnamo Jamhuri Dei alitangaza mfumo huo ungeanza Januari 2024.

Nayo Januari 2, 2024, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki akachapisha notisi kwenye Gazeti Rasmi la Serikali.

[email protected]