Serikali yajipanga kuchanja mamilioni

Serikali yajipanga kuchanja mamilioni

Na MARY WANGARI

SERIKALI imeanzisha mikakati ya kuhakikisha Wakenya milioni 30 kuanzia wenye umri wa miaka 18 wamepata dozi kamili za chanjo ya Covid-19 kufikia Desemba 2022.

Serikali inapanga kufuatilia juhudi hizo kwa mfumo wa kidijitali ili kurahisisha ukusanyaji data.

Kupitia tovuti mpya ya portal.health.go.ke, wananchi sasa wataweza kuhifadhi siku ya kwenda kupokea chanjo katika kituo kilicho karibu, kufuatilia au kuongeza maelezo yao, kuopoa cheti kinachoonyesha wamepokea chanjo na hata kupanga wakati wa kupokea dozi ya pili.

Akizungumza Alhamisi katika mkutano ulioendeshwa kwa njia ya video mtandaoni, ulioshirikisha vyombo vya habari na wadau katika Wizara ya Afya, Mkuu wa Usimamizi wa Huduma za Afya, Dkt Joseph Sitienei, alisema kuwa mfumo huo wa kidijitali kando na kurahisisha ukusanyaji data, vilevile utasaidia kupunguza makosa katika maelezo yanayotolewa.

“Makosa kama vile ya hijai ambapo unapata jina la mtu limeandikwa visivyo, kukosea tarehe au siku ya kuzaliwa, hayatakuwa kero tena kwa sababu kila mtu ataweza kujiwekea mwenyewe maelezo yake jinsi inavyofaa. Ni jambo rahisi na unaweza kutumia simu ya Smartphone, tarakilishi, kwenda Cyber Café au hata kummwomba mwenzako akusaidie kuweka maelezo yako,” alisema Dkt Sitienei.

Afisa huyo ambaye pia ni mwanachama wa Jopokazi la Kitaifa kuhusu Covid-19, alifafanua kuwa data itakayokusanywa kutokana na maelezo hayo itasaidia serikali katika mipangilio na kuwezesha kuwepo usawa katika usambazaji wa raslimali muhimu katika kukabiliana na Covid-19.

Mwenyekiti wa Jopokazi la Kitaifa kuhusu Usambazaji Chanjo, Dkt Willis Akhwale, alieleza kwamba serikali inajitahidi kuongeza idadi ya vituo vya chanjo kutoka 800 vilivyopo sasa hadi vituo 3,000 Desemba na 7,877 kufikia Juni 2022.

Alisema kuwa mikakati hiyo kuhusu Kuongeza Kasi ya Mpango wa Utoaji Chanjo inajumuisha kuongeza idadi ya vituo vya kutolea chanjo kote nchini, kuimarisha mabohari ya kuhifadhia chanjo hizo ili zidumu kwa muda zaidi na kuwezesha usafirishaji katika maeneo ya mashinani ikiwemo viwanda vya humu nchini kujaza pengo kwa kuanza kuunda chanjo dhidi ya Covid-19 na maradhi mengineyo kufikia Machi 2022.

“Malengo ya Mpango wa Kuongeza Kasi ya Utowaji Chanjo ni pamoja na kuongeza kiwango cha utowaji chanjo kutoka 40,000 kwa siku hadi 80,000 kwa siku Septemba na 150,000 kufikia Desemba, kuongeza vituo vya kutoa chanjo kutoka 800 hadi 3000 kufikia Desemba na 7,877 kufikia Juni 2022,” alisema.

Aliongeza, “Kuanzisha vituo vya uhamasishaji na utoaji chanjo kwa umma, friji 70 zenye uwezo wa kuhifadhi dozi na kujaza pengo kupitia viwanda vya humu nchini.”

Kufikia sasa, Kenya inaongoza Afrika Mashariki kwa usambazaji chanjo ambapo raia wake 1,922,085 wamepokea chanjo ikifuatiwa na Mozambique (1,394,888) Uganda (1,132,297) Malawi (768,728) na Tanzania (218, 621).

You can share this post!

Wandani wa Rais Mlimani watumia BBI kuponda Ruto

Kianjokoma: Polisi mahabusu waomba DPP azimwe