NA FARHIYA HUSSEIN
MASENETA kutoka kaunti zinazokumbwa na ukame, wamekosoa mikakati inayoendelezwa na serikali kukabiliana na hali hiyo wakisema kinachohitajika ni suluhisho la kudumu.
Kwa muda sasa, maafisa serikalini wamekuwa wakizunguka maeneo mbalimbali kusambaza vyakula vya msaada kwa waathiriwa.
Katika maeneo ya Pwani, maeneo ambapo wananchi wanakumbwa na hali ngumu kwa sababu ya kiangazi cha muda mrefu ni katika Kaunti za Kilifi, Kwale, Tana River na Lamu.Kitaifa, kaunti nyingine zinazoathirika pakubwa ni zilizo kaskazini, kaskazini mashariki, na mashariki ya nchi.
Seneta wa Tana River, Bw Danson Mungatana, alisema eneo lake linalemewa kwa vile wafugaji kutoka kaunti za nje wanaingia hadi hapo kutafuta lishe na maji, ilhali kumekauka.
“Imekuwa ngumu kwa wananchi wetu kwa vile rasilimali zetu ni chache na hazitoshi,” akasema.
Kwa upande wake, Seneta wa Kilifi, Bw Stewart Madzayo, alitoa wito wa suluhu ya kudumu.
Alisema inasikitisha kuwa tangu nchi kupata uhuru bado wanategemea kilimo cha mvua ili kutatua changamoto za ukame.
Seneta wa Mandera, Bw Ali Roba, aliitaka serikali kufanya tathmini ya dharura mara moja katika kaunti zote zilizoathirika ili kubuni mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.
Seneta wa Kitui, Bw Enoch Wambua, alisema usambazaji wa chakula cha msaada kila mara kunapokuwa na ukame si suluhu kwa matatizo yanayoshuhudiwa.
Maseneta hao walizungumza wakiwa Kaunti ya Mombasa ambapo walikuwa wamehudhuria warsha inayofadhiliwa na Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA).
“Hatua ambazo serikali ya kitaifa imechukua kukabiliana na janga la ukame si endelevu. Kama serikali, huwezi kulisha mamilioni ya watu kupitia misaada ya vyakula. Hilo si suluhu,” akasema.
Bw Wambua alipendekeza serikali kuacha kutegemea kilimo cha mvua na badala yake kuanza kuwekeza katika unyunyizaji maji.
Seneta wa Narok, Bw Ledama Ole Kina, alitaka serikali za kaunti katika maneneo kame kubadilisha bajeti zao na kuhakikisha masuala ya mabadiliko ya hali ya anga yanapewa kipaumbele.
“Sioni sababu kwa nini tujikite katika kujenga miundomsingi mikubwa wakati watu wanakufa,” alisema.
Viongozi hao wanataka serikali kwa haraka kutangaza ukame kuwa janga la kitaifa ili mataifa ya nje kutoa usaidizi wa mara moja.
Subscribe our newsletter to stay updated