Habari Mseto

Serikali yakiri wagonjwa na maiti zinazuiliwa hospitalini

March 29th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

WIZARA ya Afya, imekiri kuwa hospitali za umma na za kibinafsi zimekuwa zikiwazuilia wagonjwa wanaoshindwa kulipia gharama za matibabu.

Akizungumza Alhamisi mbele ya Kamati ya Bunge Kuhusu Afya, katibu wa wizara hiyo, Susan Mochache, alieleza wabunge kuwa wagonjwa wamekuwa wakizuiliwa bila hiari yao katika vituo vya afya, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Vilevile, katibu huyo alikiri kuwa maiti za watu ambao familia zao zilishindwa kulipa gharama za matibabu zinazuiliwa katika mochari za hospitali nyingi.

Bi Mochache alisema kwa sasa wagonjwa 300 wanazuiliwa katika hospitali za umma na za kibinafsi. Kati ya idadi hiyo, wagonjwa 184 wamezuiliwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), ambapo pia maiti za watu 387 zimezuiliwa.

“Tunajutia kuwa tulitoa habari za kupotosha kwa kusema kuwa hakuna wagonjwa ama maiti zinazozuiliwa. Baada ya uchunguzi, tumegundua kuwa visa hivi vipo, na tumewachukulia hatua maafisa katika hospitali ambazo zilitoa habari za uongo kwa wizara,” akasema Bi Mochache.

“Wizara kwa sasa inafanya mazungumzo na vituo vya afya kutafuta njia mwafaka za jinsi madeni ambayo vinadai yatalipwa,” akasema.

Katibu huyo alisema tayari wizara imevitaka vituo 3,511 vya afya kote nchini kutoa habari kuhusu visa hivyo, japo hadi jana ni hospitali 216 pekee ambazo zilikuwa zimewasilisha ripoti zao.

Vilevile, wagonjwa wanaozuiliwa wanaripotiwa kufungiwa katika vyumba ambapo ubora wake wa kiafya si mzuri, nazo maiti zikihifadhiwa katika hali duni kupindukia.

Maiti

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa KNH, Thomas Mutie, alikiri kuwa hifadhi ya maiti ya hospitali hiyo ina uwezo wa kuweka maiti 126, lakini kwa sasa mochari hiyo imerundika maiti 541.

Wizara ilieleza kamati hiyo kuwa hospitali zinadai wagonjwa na familia ambazo miili ya wapendwa wao inazuiliwa jumla ya Sh6.7 bilioni, ambapo KNH inadai Sh5.6 bilioni.

Hospitali ya Rufaa ya Moi nayo inadai Sh1 bilioni.

Wabunge walilaumu wizara hiyo kwa kushughulika na masuala ya ununuzi ya vifaa vya hospitali, badala ya kutoa huduma kwa Wakenya, wakati baadhi ya vifaa hivyo huwa havifanyi kazi.