Habari Mseto

Serikali yakosa kulipa wazee miezi 4 mfululizo

January 23rd, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MAELFU ya wazee ambao wamesajiliwa kwenye mpango wa Serikali wa kuwapa pesa za kila mwezi, hawajapokea hela hizo tangu Septemba mwaka uliopita.

Wazee hao 523,000 walio na zaidi ya miaka 70, hupokea Sh2,000 kila mwezi ambazo hulipwa kila baada ya miezi miwili.

“Mara ya mwisho tulipokea fedha hizo Septemba mwaka jana na hatujapokea maelezo yoyote kwa nini malipo hayo yamechelewa kutufikia,” akasema mzee wa miaka 77 aliyetaka jina lake lisitajwe.

Mzee huyo alisema amekuwa akihangaika kwenda benki lakini amekuwa akiambiwa pesa zimechelewa bila kupewa sababu maalum.

Kulingana na sheria zinazoongoza malipo ya fedha hizo, wazee hao hutakiwa kwenda benki binafsi ili kulipwa hela zao.

Wazee hao pia waliahidiwa kwamba wangefaidika na bima ya bure ya afya kutoka Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF), maarufu kama NHIF Inua Jamii, lakini ahadi hiyo haijatimia .

Katibu anayesimamia Idara ya Maslahi ya Jamii, Bw Nelson Marwa alisema kwamba pesa hizo zimechelewa kutokana na mchakato wa uhamisho wa teknolojia mpya ya kutuma na kupokea pesa hizo.

Kulingana na Bw Marwa, tekinolojia hiyo itahakikisha pesa hizo zitatumiwa katika akaunti za benki za jamaa za wazee hao badala ya wao kuhangaika kwenda benki kupokea fedha zao.

“Uhamisho huo wa kidijitali utakamilika mwezi huu kisha tuwalipe watu wote wanaofaidi kutokana na mpango huu wakiwemo wazee, walemavu, mayatima na wengine wenye mahitaji mbalimbali katika jamii. Watu hao watalipwa Sh8,000 kwa jumla ili kufidia miezi waliyokosa malipo,” akasema Bw Marwa.