Habari

Serikali yalenga kuangamiza TB ifikapo 2025

March 22nd, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WANANCHI wamehimizwa kuzuru hospitalini kila mara ili kukaguliwa maradhi ya Kifua Kikuu (TB), ambayo yamekuwa tishio kubwa kwa afya ya binadamu.

Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki, amesema Ijumaa kwamba serikali imejitolea kuona ya kwamba inaangamiza maradhi hayo ifikapo mwaka wa 2025 katika kaunti zote za hapa nchini.

Amesema Rais Uhuru Kenyatta, amejitolea kuona ya kwamba mipango ya kuangamiza TB inatekelezwa kwa vyovyote vile.

Bi Kariuki aliyasema hayo katika Uwanja wa Thika Stadium, wakati wa kuadhimisha kukamilika kwa matayarisho ya siku ya Kuangamiza TB ulimwenguni ambayo kilele chake itakuwa ni Machi 24 ambayo ndiyo tarehe rasmi iliyotengwa duniani.

Watu wengi ajabu wamehudhuria.

Alisema serikali inapania kuwa na vifaa maalumu aina ya Chest Radiotherapy ambavyo vitatumika  kupima kifua cha mgonjwa ili kuthibitisha ikiwa kweli ana TB au la.

Alieleza kuwa kila mwaka asilimia 40 ya TB hupatikana kwa wagonjwa wengi, huku akisema kwa miaka mingine mitano ijayo serikali inapania kuangamiza TB na ukoma kote nchini.

Alisema kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani, watu 2 milioni hufariki kila mwaka kote ulimwenguni kutokana na TB.

Waziri wa afya kaunti ya Kiambu Bi Mary Kamau alisema kaunti hiyo inafanya juhudi kuona ya kwamba inapambana na  maradhi hayo kwa vyovyote vile.

Mkewe Gavana wa Kiambu Bi Susan Ndung’u, alisema maradhi ya TB ni kati ya tano hatari yanayoangamiza watu kote nchini.

Alieleza kuwa kwa miaka mitano iliyopita wagonjwa 96,400 wametibiwa katika Kaunti ya Kiambu.

Kati ya hao 10,000 ni watoto wadogo.

Sugu

Wakati huo pia alisema ya kwamba uchunguzi unaeleza kwamba kesi 670 zimeripotiwa kuwa sugu ambazo hazipatani na dawa.

Dkt Herman Wayega, alisema watu 13 milioni kote ulimwenguni wako katika matibabu ya maradhi ya TB huku kesi 300 zikitajwa kama sugu nchini Kenya.

“Iwapo tutapata vifaa vya kisasa vya kupambana na maradhi haya bila shaka kuuangamiza ni haraka. Kila mmoja anastahili kuchukua jukumu la kujizuia kuambukizwa na maradhi hayo,” alisema Dkt Wayega.

Alisema hapa nchini Kenya kesi zipatazo 200 zimeripotiwa kutibiwa hivi karibuni huku madaktari wakiendelea kupambana  na maradhi hayo.

Mwakilishi wa shirika la Afya Duniani Dkt Richard Rudoulf alisema kuwa watu 2 milioni hufariki kila mwaka kote duniani huku wagonjwa 10,000 wakiambukizwa kila mwaka.

“Maradhi ya TB yanaweza  kuangamizwa kabisa iwapo watu watafuata masharti muhimu yanayowekwa. Iwapo mikakati  itawekwa ifaavyo bila shaka maradhi  hayo yatakuwa kama ndoto kwetu,” alisema Dkt Rudoulf.