Habari Mseto

Serikali yalenga kuhakikisha vijana wengi Kigumo wanapata ujuzi wa kozi za kiufundi

June 24th, 2020 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

KAMA njia mojawapo ya kuzima uhalifu katika kaunti ndogo ya Kigumo iliyoko katika Kaunti ya Murang’a, serikali imesema kuwa itazindua mradi wa kuwahami vijana na kozi za kiufundi.

Naibu kamishna wa Kigumo Bi Margaret Mbugua akiongea Jumatatu katika kambi ya polisi ya Muthithi, alisema kuwa kwa sasa magenge yamechipuka na kugeuza eneo hilo kuwa ngome yao, huku serikali ikijizatiti kupambana nayo.

Alisema magenge hayo yanahangaisha wenyeji kwa kuwatoza ada haramu katika sekta za kiuchumi, uvamizi wa kujeruhi na kuua na pia katika kutekeleza wizi wa mabavu.

Alitaja barabara ya Kangari hadi Kaharate ya umbali wa kilomita 42 kama mojawapo ya ngome za magenge hayo ya kikatili akisema kuwa “kabla tutafute uhusiano mwema na vijana hawa, kitu cha kwanza ni lazima tuwafunze adabu za kutii sheria.”

Alisema kuwa misako itaendelezwa sambamba na kuzinduliwa kwa mikakati ya kuwarejesha katika mkondo mwema wa kimaisha, akiwaomba wajiondoe kwa uhalifu kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

Hata hivyo, Bi Mbugua alisema utumizi wa risasi, pingu na mahakama kupambana na uhalifu miongoni mwa vijana unaweza ukawekwa breki iwapo vijana watajitolea kusalia katika utiifu wa kisheria nayo serikali iwape uwezo wa kujitafutia ajira kupitia kozi za kiufundi.

Alisema kuwa serikali huwa na wazazi wajuao pia uchungu wa mwana na ndiyo sababu haichoki kuwaomba vijana wasiwe wa kujiingiza katika mkondo hatari wa kimaisha.

Lakini alisema kuwa serikali haizingatii sana kuwavunjavunja vijana hao na kuwafunga gerezani akisema kuwa wadau wanafaa kuja pamoja na kusaka suluhu la kudumu.

“Tunafaa tujiulize ni kwa nini vijana huvutiwa na vitendo vya uhalifu na mkondo hatari wa kupambana na raia wema na serikali. Tunaweza kuwa tunawabagua katika nafasi za kujiimarisha,” akasema Bi Mbugua.

Alisema kuwa utafiti katika mataifa yaliyoimarika kiuchumi na kijamii umedhihirisha kuwa vijana ambao wameimarishwa kimasomo na kitaaluma huwa wanakwepa mtego hatari wa kujihusisha na uraibu hatari kama wa ngono kiholela, ulevi na utumizi wa mihadarati na kwa kiwango kikuu, hutii sheria.

Alisema kuwa atatumia mbinu ya kuwageuza vijana kuwa marafiki wa serikali na katika urafiki huo, vijana wawe na haya ya kukosea serikali nayo serikali ikijibu kwa kukwepa kuhujumu urafiki huo kupitia utumizi wa nguvu kujihusisha nao.

“Wakati serikali ni rafiki kwa vijana, nao vijana ni marafiki wa serikali, heshima itadumu na kila upande utajaribu juu chini kupalilia uhusiano mwema, serikali ikiwapa marafiki hao nafasi za kujiimarisha nao wakisaidia serikali kuweka amani,” akasema.

Katika hali hiyo, Bi Mbugua alisema ataweka mikakati ya ushirika na taasisi za masomo ya kozi za kiufundi eneo hilo ili asilimia isiyopungua 90 ya vijana wasio na taaluma wajihami na kozi za kuwafaa kimaisha.