Habari za Kaunti

Serikali yamsaidia mama mlemavu kurudisha mali ya Sh2m

March 6th, 2024 2 min read

NA SAMMY KIMATU

SERIKALI imemsaidia mama mlemavu aliye na watoto sita kurejesha mali ya thamani ya zaidi ya Sh2 milioni iliyokuwa imenyakuliwa na mabwanyenye.

Wakati huo huo, polisi na maafisa wa utawala wameanzisha msako kuhusu mshukiwa mkuu katika ulaghai huo aliyetambuliwa kwa jina Daniel Mutwiri almaarufu Vaite mwenye umri wa miaka 45 na ambaye inadaiwa yuko mafichoni.

Naibu Kamishna Kaunti ndogo ya Starehe John Kisang alisema mama huyo wa umri wa miaka 48 (jina limebanwa) analazimika kujisukuma kupata riziki kwa kuuza bidhaa katika kibanda kimoja katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo.

Alisema kufutia malamishi yaliyoangaziwa na kamati ya Nyumba Kumi mtaani, Msaidizi wa kamishna wa Kaunti katika tarafa ya South B, Bw Solomon Muraguri na mwenzake, Bw Samuel Kimeu Ndambuki walishirikiana na Chifu wa eneo hilo, Bw Paul Muoki Mulinge kushughulikia swala hilo.

Bw Kisang alisema mama huyo alimiliki nyumba za kukodisha katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Mariguini za thamani ya Sh990,000.

Katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo, alikuwa na nyumba sita zilizouzwa Sh90,000 ilhali zilijengwa kwa thamani ya Sh240,000.

“Mshukiwa Bw Mutwiri aliajiriwa na mama huyo kukusanya kodi ya nyumba. Hata hivyo, kutoka mwaka 2017, Mutwiri alikuwa akiuzia watu mbalimbali nyumba zinazomilikiwa na mama huyo bila mama kujua. Ilipogunduliwa mwaka huu na tukafuatilia, tulipata Bw Vaite ameuza nyumba kadhaa kwa mabwanyenye tofauti,” Bw Kisang akaambia Taifa Leo.

Linalotia uchungu zaidi, Bw Kisang alieleza ni kwamba mama huyo alijenga nyumba zingine katika mtaa wa mabanda wa Mukuru- Kisii mwaka 2017 lakini ajabu ni kwamba Vaite aliuza nyumba zote sita mwaka jana.

“Kuna visa nne vya rekodi za polisi katika kitabu cha kupiga ripoti-O.B za mlalamishi kuhusiana na matukio yote ndiposa mshukiwa anatafutwa na polisi ili ashtakiwe kulingana na mujibu wa sheria za Kenya,” Bw Kisang akasema.

Vilevile, Bw Kisang ametoa onyo kali kwa matapeli wanaonyang’anya wengine mali yao kwa njia za udanganyifu kwamba mkono wa sheria utawakamata na kuja kujutia makosa yao.

“Tuna wajibu wa kulinda mali na watu na pia watu wana haki ya kumiliki mali kwa njia ya kihalali bora sheria inakumbatiwa,” Bw Kisang asema.

[email protected]