Serikali yanyenyekea kuhusu amri kwa makanisa

Serikali yanyenyekea kuhusu amri kwa makanisa

Na MARY WAMBUI

SERIKALI Jumatatu ililazimika kukutana na viongozi wa kidini baada ya kuweka masharti makali yaliyoonekana kukandamiza uhuru wa kuabudu katika kaunti 13.

Hatua hiyo ilijiri siku chache tu baada ya serikali kupiga marufuku mikusanyiko ya ibada katika kaunti za Busia, Vihiga, Kisii, Nyamira, Kakamega, Kericho, Bomet, Bungoma, Trans Nzoia, Kisumu, Siaya, Homa Bay na Migori.

Marufuku hiyo iliibua hisia mseto kote nchini huku wakazi wengi katika maeneo husika wakikosoa hatua ya kukataza ibada ilhali taasisi nyinginezo zilikuwa zikiendelea na shughuli zao kama kawaida.

Huku ikionekana kulegeza kamba kuhusu agizo lake la awali, serikali kupitia Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i, ilitangaza jana kwamba, imejitolea kuhakikisha shughuli za ibada zinaendelea katika kaunti zilizoathirika.

“Tutathmini upya mikakati hii chini ya Wizara ya Afya ili kuona ni vipi tunavyoweza kurejelea upesi shughuli za ibada katika kaunti 13 huku tukizingatia mikakati tuliyopewa ili kuokoa maisha ya watu wetu,” alisema Dkt Matiang’i.

Dkt Matiang’i alihimiza mashirika ya kulinda usalama yanayowahangaisha viongozi wa kidini kuwaheshimu wanapoendesha shughuli zao katika sehemu mbalimbali nchini.

“Idadi kubwa ya viongozi wetu wa kidini wana heshima kuu kwa serikali na ninawahimiza machifu wote, manaibu wa chifu na maafisa wote kote nchini kuunda mahusiano thabiti na viongozi wetu wa kidini, wawape heshima na msaada wanaohitaji wanapohudumia mahitaji ya kiroho,”alisema.

Isitoshe, alitangaza kuwa serikali imeongeza muda wa hatamu ya Baraza la Makundi ya Kidini linalohusika na mikakati ya kukabiliana na janga la Covid-19 kwa muda wa miezi sita.

You can share this post!

Imara United yalenga kupandishwa daraja muhula ujao

AFYA: Je, virusi vya HIV vinachochea corona?