Serikali yanyonga wanyonge

Serikali yanyonga wanyonge

Na PAUL WAFULA

MAISHA ya Wakenya yatakuwa magumu zaidi hivi karibuni baada ya serikali ya Jubilee kuruhusu Shirika la Fedha Duniani (IMF) kurudi nchini kwa masharti makali ya kusimamia uchumi.

Wataalamu wa uchumi wanasema Wakenya wanafaa kuanza kujiandaa kwa nyongeza zaidi ya ushuru, maelfu ya watumishi wa serikali na mashirika ya umma kufutwa kazi na kupanda kwa bei za bidhaa.

Hatua hii imekuja mwongo mmoja baada ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki kufifisha usemi wa IMF kuhusu usimamizi wa uchumi alipopunguza ukopaji wa kiholela kutoka mataifa ya kigeni, pamoja na usimamizi bora wa uchumi.

Masharti makali ya IMF yatakuwa pigo kubwa kwa mamilioni ya Wakenya ambao tayari wamelemewa na bei za juu za bidhaa muhimu kama vile vyakula, mafuta taa, petroli, umeme na nauli kutokana na ushuru wa juu kupindukia.

Mwezi uliopita serikali ilipuzilia mbali kilio cha Wakenya baada ya kuongeza bei ya petroli hadi Sh122 kwa lita moja, msemaji wa serikali, Cyrus Oguna akisema ni muhimu ushuru kuwa wa juu kwa ajili ya kufadhili shughuli za serikali na maendeleo

Umeme nao umekuwa wa gharama ya juu kutokana na kampuni ya Kenya Power kutoza ada za juu ili kulipa kampuni za kuzalisha umeme, ambazo kulingana na mkataba sharti zilipwe hata kama hakuna umeme Kenya Power imenunua kutoka kwao.

Hii imesababisha bei ya umeme kuendelea kuwa ya juu licha ya uwekezaji mkubwa katika uzalishaji wa kawi nchini.

Wakenya pia wanaendelea kufinywa, ambapo wiki iliyopita, Benki Kuu (CBK) iliruhusu benki na mashirika ya akiba na mikopo (Sacco) kuanza kutoza ada kwa shughuli za kifedha kwa simu kwa kiasi kinachozidi Sh100.

Mambo yamekuwa magumu zaidi kutokana na hatua za kukabili Covid-19 ambazo zimetangazwa bila mpango wowote wa serikali wa kutoa afueni kwa waliopoteza kazi kama vile wahudumu wa matatu na mabasi, wanaotoa huduma za kitalii, wahudumu wa kampuni za ndege na wamiliki na wafanyikazi wa mikahawa na mabaa.

Mbali na Covid, kumekuwa na hali mbaya ya kibiashara nchini hasa kwa biashara ndogo, ambapo nyingi zimefungwa na zingine kunadiwa mali yao kwa kushindwa kulipia mikopo.

Baada ya IMF wiki iliyopita kukopesha Kenya Sh257 bilioni, sasa shirika hilo litakuwa na usemi mkubwa kuhusu usimamizi wa uchumi kwa matakwa yasiyojali maslahi ya mwananchi wa kawaida.

Mkopo huo umeongeza deni linalodaiwa Kenya kuzidi Sh8 trilioni, na kutumbukiza nchi katika tatizo kubwa zaidi la kulipa deni hilo kubwa.

Kumekuwa na wasiwasi huenda Kenya ikapoteza baadhi ya raslimali zake kuu kwa wakopeshaji hao hasa Bandari ya Mombasa.

Kulingana na masharti ambayo IMF imepatia Kenya, serikali haitakuwa na budi ila kuongeza ushuru ili kutii agizo la shirika hilo kuhusu kupunguza ukopaji katika kufadhili shughuli zake.

Sharti lingine ni kubinafsishwa kwa mashirika ya serikali, hatua ambayo itaambatana na kupunguzwa kwa idadi ya wafanyakazi.

IMF pia inataka Kenya kupunguza bajeti yake ya kila mwaka, jambo ambalo huenda likatatiza miradi ya maendeleo.

Katika utawala wa marehemu Daniel Moi, maelfu ya watumishi wa umma walifutwa kazi katika mpango uliosukumwa na IMF. Utozaji wa ada za hospitali na shule pia ulianza wakati huo.

Mzee Kibaki alifanikiwa kubadilisha hali hiyo kwa kupunguza ukopaji, jambo lililomwezesha kuwa na uhuru wa kusimamia uchumi bila masharti ya wageni.

Lakini mafanikio hayo sasa yamekuwa historia, baada ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto kubadilisha mkondo wa usimamizi uchumi wa Mzee Kibaki na badala yake wakaanza kukopa kila uchao.

Ongezeko la ufisadi na kutumiwa kwa miradi ya umma kwa manufaa ya maafisa binafsi wa serikali na wafanyibiashara pia kumevuruga uchumi wa nchi, huku juhudi zilizoanzishwa 2018 za kupambana na ufisadi zikifeli.

You can share this post!

Zaidi ya wafungwa 1,800 watoroka baada ya shambulio la...

Tumieni pesa za refarenda kulisha raia – wabunge